Katika hatua inayoonesha ni ya kuzidi kuunga mkono juhudi za kuleta amani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema kuwa Nairobi iko tayari kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa sekta ya umma wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kama sehemu ya kuisaidia nchi hiyo kuwa na utulivu wa kudumu na watu wake kuishi kwa usalama na amani.
Ahadi hizo za Rais Kenyatta zimetolewa baada ya kukutana na rais mpya wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi. Itakumbukwa kuwa Rais Uhuru Kenyatta ndiye kiongozi pekee wa nchi aliyehudhuria sherehe za kuapishwa Felix Tshisekedi Tshilombo, kuwa rais mpya wa DRC.
Katika hatua inayoonekana ni ya kulipa fedhila, rais huyo mpya wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameichagua Kenya kuwa nchi ya kwanza ya Afrika Mashariki kuitembelea baada ya kuapishwa kuwa rais wa DRC.
Kabla ya Kenya, Rais Tshisekedi alitembelea pia Angola juzi Jumanne ikiwa ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu achaguliwe kuwa Rais wa DRC na leo mchana ametembelea pia nchi jirani ya Congo Brazzaville.
Miongoni mwa wanasiasa maarufu alioonana nao akiwa Nairobi, ni mkuu wa upinzani wa Kenya, Raila Odinga ambaye hivi sasa amekuwa akishirikiana vizuri na Rais Uhuru Kenyatta na kuacha uhasama wa kisiasa.
Itakumbukwa kuwa hata Raila Odinga wa chama cha ODM na Kalonzo Musyoka wa chama cha Wiper nchini Kenya nao alihudhuria sherehe za kuapishwa Rais Felix Tshisekedi Tshilombo mwezi uliopita wa Januari, suala ambalo linaonesha ni kiasi gani rais huyo mpya wa DRC alivyo na uungaji mkono wa wanasiasa wa Kenya, iwe ni serikali au wapinzani.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇