Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii imelitaka Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kuacha kufungia nyimbo za wasanii na badala yake kutekeleza jukumu la kuwalea na kuwashauri kuandaa nyimbo zinazoendana na maudhui.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kamati hiyo bungeni jijini Dodoma leo Alhamisi Februari 7, 2019 makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Juma Nkamia amesema mojawapo ya kazi ya Basata ni kutoa ushauri na misaada ya kiufundi kwa wasanii na wadau.
Amesema hivi karibuni kumekuwa na wimbi la kufungia nyimbo za wasanii na matamasha mbalimbali.
Amesema wasanii hao wamekuwa wakipata mapato mengi kutokana na ‘Hits’ wanazopata kupitia mitandao ya kijamii kama Youtube, Serikali haipati chochote kutokana na mahusiano yasiyoridhisha.
Nkamia amesema kamati inapendekeza Basata kutekeleza jukumu lake la kuwalea pamoja na kuwashauri kuandaa nyimbo zinazoendana na maudhui na kuwaonya pale wanapokosea.
Amesema kamati inashauri kuboresha mahusiano na wasanii ili kufaidika na mapato yatokanayo na hits za mitandao ya kijamii.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇