Hatimaye Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imemwachia huru rais wa zamani wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo baada ya vuta nikuvute kati ya mawakili wa mwanasiasa huyo na Waendesha Mashitaka wa ICC.
Jaji wa mahakama hiyo, Chile Eboe-Osuji amesema Gbabgo na mpambe wake Charles Ble Goude wanapaswa kuachiliwa ili kulinda hadhi ya mchakato wa kesi ya mahakama hiyo.
Wawili hao waliachiwa huru jana usiku na kupelekewa kusikojulikana.
Kabla ya kuachiwa, Mwendesha Mashitaka mwandamizi wa ICC, Helen Brady amewaambia majaji wa ICC kuwa, wana wasiwasi kwamba huenda Gbabgo na mpambe wake Charles Ble Goude wasirejee katika mahakama hiyo iliyoko mjini The Hague nchini Uholanzi iwapo majaji wa ICC watatoa uamuzi wa kusikilizwa upya kesi zao.
Wakili wa Gbagbo, Emmanuel Altit alisisitiza kuwa mteja wake alipaswa kuachiwa huru mara moja bila masharti yoyote na aruhusiwe kurejea nchini kwake haraka iwezekanavyo.
Hata hivyo Waendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ambao walikata rufaa kupinga uamuzi wa wawili hao kuachiwa huru, wanataka waachiwe huru na kisha wapelekwa katika nchi jirani na Uholanzi, sambamba na kutwaliwa pasi zao za kusafiria.
Wawili hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka ya jinai dhidi ya binadamu katika mwaka 2010-2011 katika vita vya ndani Kodivaa ambapo watu 3,000 waliuawa.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇