Jan 26, 2019 02:58 UTC
Umoja wa Mataifa umewaarifisha wajumbe wa timu yake ya kimataifa itakayochunguza mauaji ya mwandishi habari mkosoaji wa utawala wa Al Saud.
Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa jana Ijumaa ilitoa taarifa na kutangaza kuwa timu hiyo ya wataalamu wa kimataifa itachunguza mauaji ya Jamal Khashoggi mwandishi habari mkosoaji wa utawala wa Saudi Arabia. Agnes Callamard Ripota wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia mauaji ya kiholela na kinyume cha sheria amesema kuwa yeye ndiye atakayeiongoza timu hiyo; na kwamba kuanzia Januari 28 hadi tarehe tatu Februari ataelekea Uturuki kwa lengo hilo.
Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa aidha imetangaza kuwa katika safari yake hiyo nchini Uturuki Bi Agnes Callamard ataongozana na wataalamu wengine wawili kwa majina ya Helena Kennedy na Duarte Nuno Vieira. Jamal Khashoggi mwandishi habari mkosoaji wa utawala wa Aal Saud aliuawa mwezi Oktoba mwaka jana ndani ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia huko Istanbul Uturuki.
Mashirika ya Ujasusi ya Marekani na Uturuki yamethibitisha kuhusika mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia Muhammad bin Salman katika mauaji hayo ya kutisha.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇