Utekelezaji wa Serikali Mtandao ni moja ya sehemu muhimu ya maboresho
yaliyofanyika katika utumishi wa umma, ambao umesaidia kurahisisha utoaji wa
huduma katika taasisi za umma zinazopatikana kwa urahisi, kwa wakati na kwa
gharama nafuu kwa kutumia TEHAMA.
Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Mkurugenzi Idara ya Ushauri na Uchambuzi
Kazi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Mick Kiliba kwa niaba
ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma wakati akifungua
kikao kazi cha pili cha Serikali Mtandao chenye lengo la kuwakutanisha wadau
wanaohusika na utekelezaji wa Serikali Mtandao kwa ajili ya kujenga uwezo,
kuongeza ushirikiano na kubadilishana uzoefu ikiwa ni pamoja na kujadiliana
njia sahihi za kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa
Serikali Mtandao.
Bw. Kiliba amefafanua kuwa, utekelezaji wa Serikali Mtandao, umechangia kwa
kiasi kikubwa katika kurahisisha utoaji wa taarifa na huduma nyingine kwa
wananchi kwa haraka, uwazi, gharama nafuu wakati wowote na kuongeza kuwa,
Serikali Mtandao ni kichocheo muhimu katika kufikia Dira ya Taifa ya Mwaka 2025
inayolenga pamoja na mambo mengine, kufikia maendeleo ya viwanda.
Bw. Kiliba ameongeza kuwa, utekelezaji wa Serikali Mtandao umejikita katika
kuboresha utoaji wa huduma miongoni mwa taasisi za umma, kati ya taasisi za
umma na wananchi, kati ya taasisi za umma na sekta ya biashara na kwa serikali
kuwahudumia watumishi.
Bw. Kiliba ameainisha kuwa, utekelezaji wa Serikali Mtandao unalenga
kuimarisha utawala bora na kuongeza tija na ufanisi katika uendeshaji wa
taasisi za umma kwa kuhakikisha uwepo wa mawasiliano ya haraka, yenye uhakika
na salama ndani na kati ya taasisi mbalimbali za serikali.
Aidha, Bw. Kiliba ametoa wito kwa washiriki kuelekeza majadiliano katika
kauli mbiu ya kikao kazi hicho inayosema “Uwianishaji
wa Rasilimali za TEHAMA kwa Maendeleo ya Viwanda” ambayo imelenga kuonyesha
umuhimu na nafasi ya TEHAMA katika maendeleo ya viwanda nchini.
Bw. Kiliba amesisitiza kuwa, kauli mbiu hiyo inatukumbusha kwamba ukuaji wa
viwanda nchini unategemea pamoja na mambo mengine, uwezeshaji wa TEHAMA, ambao
unasaidia upatikanaji wa taarifa sahihi na kwa wakati ili kuwezesha kufanya
maamuzi sahihi na kwa haraka ikiwa ni pamoja na wananchi kupata huduma
mbalimbali kama vile uanzishaji wa biashara na uombaji wa vibali mbalimbali.
Kikao kazi hiki cha pili cha kundi la kwanza kinahudhuriwa na Maofisa
TEHAMA, Maofisa Ununuzi, Maofisa Mawasiliano Serikalini, Maofisa Utumishi,
Maofisa Utawala, Wakaguzi, Wahandisi, Wahasibu, Maofisa Mipango na watumiaji wa
mifumo ya TEHAMA.
IMETOLEWA
NA;
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
OFISI YA RAIS (UTUMISHI)
TAREHE 30 JANUARI, 2019
Mkurugenzi Idara ya Ushauri na Uchambuzi Kazi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Mick Kiliba akifungua rasmi kikao kazi cha
Serikali Mtandao kwa niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
utumishi wa Umma katika ukumbi wa Chuo cha Sayansi ya Kompyuta, Habari na
Mawasiliano uliopo Chuo Kikuu Dodoma mapema
Mkurugenzi Idara ya Ushauri na Uchambuzi Kazi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Mick Kiliba (katikati mstari wa mbele)
akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Wakala ya Serikali Mtandao pamoja
na washiriki wa kikao kazi cha Serikali Mtandao mara baada ya kufungua rasmi
kikao kazi cha Serikali Mtandao kwa niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya utumishi wa Umma katika ukumbi wa Chuo cha Sayansi ya Kompyuta,
Habari na Mawasiliano uliopo Chuo Kikuu Dodoma mapema leo
Baadhi ya washiriki wa kikao kazi cha Serikali Mtandao wakimsikiliza
Mkurugenzi Idara ya Ushauri na Uchambuzi Kazi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma, Bw. Mick Kiliba (hayupo pichani) wakati akifungua kikao kazi hicho kwa
niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya utumishi wa Umma katika
ukumbi wa Chuo cha Sayansi ya Kompyuta, Habari na Mawasiliano uliopo Chuo Kikuu
Dodoma mapema
Mkurugenzi Idara ya TEHAMA Serikalini, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Priscus Kiwango akitoa neno la shukrani na
kuahidi kutekeleza maelekezo ya mgeni rasmi baada ya ufunguzi wa kikao kazi cha
Serikali Mtandao katika ukumbi wa Chuo cha Sayansi ya Kompyuta, Habari na
Mawasiliano uliopo Chuo Kikuu Dodoma mapema leo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇