Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula amekerwa na makusanyo madogo ya mapato katika halmashauri mbalimbali nchini kupitia kodi ya ardhi.
Akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi wa Halmashauri za Mji na Wilaya ya Geita jana mkoani Geita alipofanya ziara ya kushtukiza kufuatilia utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa katika halmashauri hizo, Dk Mabula alisema, mapato ya sekta ya ardhi katika halmashauri nyingi hayaridhishi na kueleza kuwa halmashauri nyingi mapato yake yako chini ya asilimia 30.
Alisema pamoja na halmashauri hizo kuwa na mapato kidogo kupitia sekta ya ardhi lakini watendaji wake hawaoneshi jitihada zozote kuhakikisha wanakusanya mapato ya kutosha kupitia sekta hiyo na hivyo aliwataka watendaji hao kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato kwa kuwa msisitizo wa serikali ya awamu ya tano ni kukusanya kodi.
‘’Kwa staili hii tutafika kweli? Mna bahati mbaya sasa watendaji wa sekta ya ardhi katika halmshauri mtakuwa chini ya wizara moja kwa moja na rais amepiga kelele kuhuisiana na kodi ninyi mnarelax’’ alisema Dk mabula.
Hata hivyo, Dk Mabula aliisifu halmashauri ya Mji wa Geita kwa kukusanya mapato kwa zaidi ya asilimia sitini. Kwa Mujibu wa taarifa ya Halmshauri ya Mji wa Geita, kuanzia mwezi Julai hadi Oktoba 2018, halmashauri hiyo imekusanya jumla ya shilingi 389,699,937.28 kati ya milioni 600,000,000 ilizopanga kukusanya.
Kwa upande wake Halmashauri ya Wilaya ya Geita kupitia, Afisa Ardhi wake Faraja Kaluwa pamoja na halmashauri hiyo kupewa malengo ya kukusanya milioni 150 lakini kufikia desemba 2018 imefanikiwa kukusanya shilingi milioni 12,480,500 tu.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliwataka wakuu wa idara za ardhi katika halmashauri za Mji na Wilaya ya Geita kutoa ahadi ya utekelezaji maagizo aliyoyatoa na hatua gani zichukuliwe kwao iwapo maagizo hayatatekelezwa kwa wakati.
Maagizo aliyoyatoa Dk Mabula ni kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ya kodi ya ardhi, uingizaji viwanja na mashamba katika mfumo wa kielektronik, utoaji hati za ardhi pamoja na utoaji hati za Madai (demand notes) kwa wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi.
Aidha, Dk Mabula ameziagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha zinaingiza viwanja na mashamba kwenye mfumo wa malipo kwa njia ya kielektronik na kutaka kasi ya utoaji hati kuongezeka ili kuwawezesha wananchi kiuchumi na wakati huo kuiingizia serikali mapato kupitia kodi ya ardhi.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula amezitaka halmashauri nchini kuhakikisha zinatoa leseni za makazi katika maeneo yenye nyumba zilizojengwa nje ya urasimishaji na mipango Miji na kueleza kuwa zoezi hizo linatakiwa kukamilika mwezi machi mwaka huu.
Dk Mabula amezitaka Halmashauri kuanisha maeneo yote ya nyumba hizo na kupatiwa leseni za makazi kwa gharama ya shilingi 5000 sambamba na kuziingiza katika kumbukumbu za halmashauri na kubainisha kuwa leseni hizo ni hatua za kuelekea wamiliki wake kupatiwa hati.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇