Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umefungua kesi Mahakama Kuu ya Arusha, kutaka iwalazimishe polisi kuwapeleka mahakamani watuhumiwa watano wa Loliondo, waliowekwa mahabusu kwa siku saba
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, alidai watetezi wa haki za binadamu Clinton Kairungi, Supuk Maoi, Manyara Kaita na wananchi wengine wawili walikamatwa na polisi Janauri 7, mwaka huu.
“Ikumbukwe kwamba kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya Mwaka 1985, mtuhumiwa anapokamatwa, anakuwa na haki mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuambiwa kosa analotuhumiwa nalo, kupewa dhamana, kuonana na ndugu, kupelekwa mahakamani kwa wakati pamoja na kuelezwa haki yake ya kupata msaada wa kisheria," alisema na kuongeza:
“Hata hivyo, watetezi hawa baada ya kukamatwa na Jeshi la Polisi, hawakupatiwa haki yoyote ile kati ya haki zilizotajwa kwa mujibu wa sheria. THRDC ilimpeleka Wakili Samson Rumembe, pamoja na Msaidizi wa Kisheria ndugu Charles Nangoya, kwenda kuwapa msaada wa kisheria, lakini walizuiwa na Jeshi la Polisi hata kuwaona watuhumiwa hao.”
Olengurumwa alisema Wakili Rumembe alipouliza kosa wanalotuhumiwa nalo watuhumiwa, polisi pia hawakutaka kuonyesha ushirikiano na hivyo jitihada za kuwasaidia kupata dhamana zikagonga mwamba.
Alisema: “Mpaka sasa tunavyoongea, watetezi hawa bado wako rumande, jambo ambalo ni kinyume cha Kifungu cha 64(1)(c) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya Mwaka 1985, ambayo inaelekeza polisi kukaa na mtuhumiwa kwa saa zisizozidi 24 kabla ya kuwapa dhamana ya polisi au kuwapeleka mahakamani kwa mujibu wa sheria.”
Akizungumzia hali ya ukiukwaji wa haki za binadamu Loliondo, alisema imeendelea kuwa mbaya siku hadi siku kwa kuwa kuna uharibifu wa mali, ukiukwaji wa haki za binadamu, watu kukamatwa na kuweka mahabusu bila kufikishwa mahakamani.
“Watetezi wa haki za binadamu ambao wapo mstari wa mbele kutetea haki za raia Ngorongoro, wamekuwa wakikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kughushi, ambapo mpaka sasa wapo baadhi ya watetezi Loliondo bado wa wana kesi mahakamani,” alidai.
Kwa mujibu wa Olengurumwa, mwaka 2016, Supuk Maoi na mwenzake Clinton Mshao, walifunguliwa mashataka ya kughushi kwa kutuhumiwa kwa kosa la ujasusi (espionage), lakini walishinda kesi baada ya kupata msaada wa kisheria na kwamba chanzo cha mitafuruku yote ni msimamo wa wanachi na watetezi juu ya mikakati ya siku nyingi ya kutaka kuchukua eneo la wananchi (OSERO) na kuikabidhi moja kwa moja Kampuni ya Uwindaji ya Kiarabu (OBC).
“Katika kipindi chote ambacho mgogoro wa ardhi Loliondo umedumu, tumeshuhudia Jeshi la Polisi likitumia nguvu kubwa kuwashuhulikia watetezi wa haki za binadamu pamoja na raia, huku wakibambikiziwa kesi mbalimbali,” alisema.
Olengurumwa alilitaka Jeshi la Polisi kuwaachia mara moja watuhumiwa hao pamoja na wengine waliokamatwa bila masharti yoyote au wawafikishe mahakamani ili wakakabiliane na mashtaka dhidi yao.
“Pia tunamwomba IGP kuwachukulia hatua OCD wa Ngorongoro pamoja na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha kwa kukiuka utaratibu wa Jeshi la Polisi pamoja na sheria za nchi, ili iwe fundisho wa wengine wanaokiuka,” alisema.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇