Mlinzi wa zahanati ya Kijiji cha Katani, Kata ya Nkandasi wilayani Nkasi mkoani Rukwa Laudifasi Sokoni (60) amejinyonga katika chumba cha kuchomea wagonjwa sindano cha Zahanati hiyo kwa kutumia shuka lake.
Tukio hilo lilibainika asubuhi ya Januari 23,2019 muda mfupi baada ya wahudumu kufika kazini kwa ajili ya kuanza maandalizi ya kutoa huduma.
Akizungumzia tukio hilo Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Jofrey Kisato alisema baada ya wahudumu wa zahanati hiyo kufika kazini na kuanza kuandaa mazingira ya kutoa huduma ndipo walipogundua tukio hilo hali iliyosababisha watoe taarifa kwenye uongozi wa kijiji nao ukatoa taarifa kituo cha polisi.
Alisema marehemu alikuwa ni mlinzi wa Zahanati ya Kijiji na kuwa alikuwa akiishi peke yake kwa muda mrefu kutokana na mkewe kufariki dunia na mpaka sasa hawajui chanzo cha yeye kuamua kujinyonga.
“Inaonekana alidhamiria kujinyonga kwani alikwenda eneo lake la lindo na shuka, usiku wa kuamkia siku hiyo aliamua kujitundika kwa kutumia shuka hilo na wahudumu wa Zahanati hiyo waligundua mwili wake ukining’inia wakati wakiandaa mazingira ya kutoa huduma hali iliyosababisha baadhi ya wagonjwa kuingiwa hofu na kutimua mbio bila kupata huduma,” alisema mwenyekiti wa kijiji hicho.
Kwa upande wake Kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa George Kyando alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa marehemu hakuacha ujumbe wowote. Alisema baada ya polisi kufanya uchunguzi wa awali walibaini kuwa chanzo cha marehemu kufikia maamuzi hayo ni kutokana na kukabiliwa na maisha magumu pamoja na upweke.
Kamanda Kyando alisema tangu mke wa marehemu kufariki dunia mlinzi huyo alibaki akionekana kuwa na msongo wa mawazo pamoja na hali ngumu ya maisha inayomkabili ndiyo sababu zilizopelekea kujinyonga. Alisema pamoja na kuwepo kwa sababu hizo za awali lakini polisi wanaendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo hasa cha Sokoni kufikia maamuzi ya kujinyonga.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇