Bi. Marzieh Hashemi, mtangazaji wa kanali ya Press TV ya Iran, amesema kuwa alikamatwa nchini Marekani kutokana na imani yake ya Uislamu.
Bi Hashemi ambaye alikuwa kizuizini nchini Marekani ameyasema hayo katika mahojiano na Shirika la Habari la Associated Press na kusema kuwa, sababu ya kushikiliwa kwake ni kazi yake ya uandishi wa habari na imani yake. Mwandishi huyo wa habari na mtangazaji wa kanali ya habari ya Press TV ameyasema hayo baada ya kuachiliwa huru kutoka korokoroni alikokuwa anazuiliwa nchini Marekani. Akiashiria juu ya nara ya Rais Donald Trump wa Marekani ya 'Tuifanye tena Marekani kuwa kubwa' amesema: "Sijui malengo ya nara ya kuifanya tena Marekani kuwa kubwa ni gani, lakini iwapo lengo lake ni kuwapokonya wananchi haki zao za kimsingi kila siku, kwa mtazamo wangu, sio kuifanya Marekani kuwa kubwa."
Bi. Marzieh Hashemi ameongeza kwa kusema: "Ninaamini kupaza sauti juu ya haki na ukweli. Ninaamini kufikisha sauti ya watu wanaodhulumiwa na jambo hilo linapingana na siasa za madola ya kibeberu, na sehemu kubwa ya yaliyotokea inahusiana na suala hilo." Bi. Marzieh Hashemi aliachiliwa huru jioni ya Jumatano kwa majira ya Washington baada ya kushikiliwa kizuizini na serikali ya Marekani kwa muda wa siku 11 bila ya kutolewa tuhuma zozote dhidi yake.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇