LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 29, 2019

MAJAJI WALAIOTEULIWA JUZI WAAPISHWA LEO IKULU JIJINI DAR ES SALAAM

IKULU, DAR ES SALAAM
RAIS Dk. John Magufuli leo, amewaapisha Majaji sita wa Mahakama ya Rufani na Majaji 15 wa Mahakama Kuu aliowateua juzi, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kuwaapisha viongozi hao na kushuhudia wakila kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Harold Nsekelakatika hafla hiyo, Rais Magufuli ameiahidi kuwa ataendelea kuteua Majaji wengine ili kukabiliana na upungufu wa Majaji uliopo kadiri uwezo wa kifedha utakavyoruhusu, na amewataka Majaji waliopo pamoja na Mahakimu kuendelea na mpango wa kukabiliana na changamoto za Mahakama zilizopo.

Rais Magufuli amewapongeza Majaji wote aliowateua na kuwataka kwenda kuchapa kazi ya kutoa maamuzi yenye kuzingatia haki kwa wananchi.

Amepongeza Majaji na Mahakimu ambao wamekuwa wakitekeleza wajibu wao kwa kusimamia sheria na haki na ametoa wito kwa Mahakama kuhakikisha maeneo yanayolalamikiwa yanarekebishwa ikiwemo jamii kushuhudia watu wanaokabiliwa na mashtaka yenye ushahidi wa dhahiri wakiachiwa huru.

Majaji wa Mahakama ya Rufani walioapishwa ni Winfrida Beatrice Korosso, Barke Mbarak Aboud Sehel, Lugano Samson Mwandambo, Dk. Mary Caroline Levira, Ignas Paul Kitusi na Rehema Kerefu Sameji.

Majaji wa Mahakama Kuu walioapishwa ni John Rugalema Kahyoza, Susan Bernard Mkapa, Fahamu Hamidu Mtulya, Cyprian Phocas Mkeha, Willbard Richard Mashauri, Dunstan Beda Ndunguru, Seif Mwinshehe Kulita, Upendo Elly Madeha, Yohane Bokobora Masara, Mustapha Kambona Ismail, Athuman Matuma Kirati, Zephrine Nyalugenda Galeba, Dk. Ntemi Nimilwa Kilekamajenga, Dk. Juliana Laurent Masabo na Dk. Lilian Mihayo Mongella.


Kwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri, Rais Magufuli amewataka kwenda kufanya kazi kwa ushirikiano na kujiepusha na matumizi mabaya ya mamlaka waliyonayo, pia amewataka kuhakikisha wanasimamia ipasavyo ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Katika salamu zake Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa uteuzi wa Majaji hao wakiwemo Majaji wanawake 4 wa Mahakama ya Rufani na Majaji wanawake 4 wa Mahakama Kuu na amewataka Majaji wote kwenda kufanya kazi ya kutoa haki vizuri.

Pamoja na kumshukuru Rais Magufuli kwa kuteua Majaji wapya, Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi ametoa mwito kwa Mahakama kutekeleza mpango wa kuanzisha Mahakama zinazotembea (Mobile Courts) ili kupeleka huduma za Mahakama karibu zaidi na wananchi, na pia amewasihi Majaji hao kujiepusha na vitendo vya rushwa ambavyo vinaangamiza haki.

Jaji Mkuu Prof. Ibrahim Hamis Juma amemshukuru Rais Magufuli kwa uteuzi wa Majaji hao ambao umeiwezesha Mahakama kuongeza idadi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani kutoka 14 hadi 20 na Majaji wa Mahakama Kuu kutoka 66 hadi 81, kupunguza uwiano wa mashauri yanayosikilizwa na Majaji kwa mwaka kutoka Jaji mmoja kusikiliza mashauri 568 hadi kufikia Jaji mmoja kusikiliza mashauri 463 na kwamba itasaidia utekelezaji wa mpango wa kila Jaji kusikiliza mashauri 220 kwa mwaka.

Amemuomba Rais Magufuli kuendelea kuteua Majaji zaidi hasa wakati huu Mahakama inapotekeleza mpango wake wa maendeleo ambapo kuna ujenzi wa Mahakama za Mwanzo 12 na majengo mengine 36 yatakayokamilika katikati ya mwaka huu, na ujenzi wa Mahakama za Wilaya 28 ambazo zitahitaji watumishi.

Hafla ya kuapishwa kwa Majaji hao imehudhuriwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Jaji Mkuu Prof. Ibrahim Hamis Juma, Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi, Majaji Wakuu na Majaji Viongozi wastaafu, Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu, Majaji wastaafu viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa Dini, viongozi wa taasisi mbalimbali zinazohusiana na masuala ya sheria pamoja na Wakuu wa Wilaya wawili na Wakurugenzi 10 wa Halmashauri.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages