Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na mradi wa Little Hearts wa nchini Saudi Arabia ambao ni moja ya mradi wa Afya ulioko ndani ya Taasisi ya Msaada ya Muntada yenye makao Makuu yake mjini London nchini Uingereza wamefanya matibabu ya moyo kwa watoto 72.
Matibabu hayo yamefanyika katika kambi maalum ya siku saba ya matibabu ya moyo kwa watoto wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu ya moyo kutopitisha damu vizuri. Umri wa watoto hao unaanzia miezi sita hadi miaka 31.
Katika kambi hiyo ilianza tarehe 01/12/2018 na kumalizika leo tarehe 07/12/2018 kati ya wagonjwa 72 waliofanyiwa matibabu watoto 43 wamefanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua na 29 wamefanyiwa upasuaji wa kufungua kifua na hali zao zinaendelea vizuri na wengine wameshatoka katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) na kupelekwa wodini kwa ajili ya kuendelea na matibabu ikiwa ni pamoja na kuanza mazoezi.
Madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto wamefanya upasuaji wa kurekebisha valvu, kuziba matundu, kurekebisha mishipa ya moyo ambayo imekaa vibaya na kurekebisha mfumo wa uzungukaji wa damu katika moyo.
Kwa upande wa upasuaji wa bila kufungua kifua kupitia tundu dogo linalotobolewa katika mshipa mkubwa wa damu uliopo kwenye paja tumeweza kufanya matibabu kwa watu wazima wawili wenye umri wa miaka 31 ambao walikuwa na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambapo mmoja mshipa wake mkubwa wa moyo ulikuwa umebana na kushindwa kupitisha damu vizuri na mmoja alikuwa na tundu.
Changamoto kubwa tuliyokabiliana nazo katika kambi hii ni ufinyu wa chumba cha uangalizi maalum (ICU) kwa wagonjwa wanaotoka katika chumba cha upasuaji. Tunaamimi baada ya kukamilika kwa ukarabati wa jengo la watoto ambalo litakuwa na vitanda 41 kati ya hivi vya ICU tisa tatizo la vitanda litamalizika kwa kiasi kikubwa.
Tunatoa wito kwa wazazi na walezi wasisahau kupima afya za watoto wao pale watakapoona kuna hali ya tofauti katika ukuaji wa mtoto kwani magonjwa mengi ya moyo yanaanzia utotoni. Mtoto akianza kuugua magonjwa ya moyo wazazi wengi wanadhani ni matatizo ya kifua baada ya kumfikisha hospitali na kufanyiwa vipimo ndipo inagundulika mtoto anasumbuliwa na magonjwa ya moyo. Kwa akina mama wajawazito wafanye uchunguzi (Fetal Echocardiography) wa kuangalia kama mtoto aliyeko tumboni ana matatizo ya moyo au la.
Taasisi inawashukuru sana wenzetu hawa wa Taasisi ya Msaada ya Muntada katika mradi wake wa afya wa Little Hearts kupitia Taasisi ya Kiislamu ya DHI NUREIN yenye makao yake makuu Mkoani Iringa kwa kutuwezesha kutoa huduma ya matibabu kwa watoto wetu. Hii ni mara ya tano kwa wenzetu hawa kuja katika Taasisi yetu na kutoa huduma tangu mwaka 2015 tulipoanza kufanya matibabu ya pamoja kwa watoto ambapo jumla ya watoto 367 wamefanyiwa matibabu kati ya hawa 140 wamefanyiwa upasuaji wa kufungua kifua na 227 upasuaji wa bila kufungua kifua.
Kwa namna ya kipekee tunaishukuru sana Serikali kwa kuhakikisha tunafanya kambi maalum za matibabu ya moyo katika Taasisi yetu na hivyo wagonjwa kupata huduma za matibabu kwa wingi. Licha ya wagonjwa kupata matibabu wataalam wetu wa afya wamekuwa wakijifunza mambo mbalimbali katika kambi hizi hii ikiwa ni pamoja na kubadilishana ujuzi wa kazi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇