Amesema motisha hiyo inakwenda sambamba na uhakiki wa wafanyakazi wote wa kampuni hiyo huku akielezea namna ambavyo amefurahishwa na utendaji kazi wa wafanyakazi wote na hasa katika kumuunga mkono Rais Dk.John Magufuli ambaye amefanya mambo makubwa kwa mwaka 2018.
Akizungumza leo ofisini kwake Sungura amesema Desemba 28 mwaka huu wa 2018 amekutana na wafanyakazi wote kwa kada mbalimbali na alitumia sehemu hiyo kuelezea mikakati ya kampuni hiyo ambayo imedhamiria kufanya mambo makubwa. "Tulipokutana na wafanyakazi kuna mambo mengi ambayo tumeyazungumza.
Pia nilitumia nafasi hiyo kuwashukuru kwa kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayofanya.
Rais wetu amefanya mambo makubwa kwa mwaka huu yakiwamo ya kuboresha sekta ya anga, miundombinu kwa upanuzi wa barabara na ujenzi wa madaraja, umeme wa mto Rufiji, ununuzi wa korosho, elimu bure na mambo mengine mengi ambayo yamefanyika.Hivyo wafanyakazi hawa wamekuwa wakiunga mkono kwa vitendo jitihada za Rais,"amefafanua. Ameongeza wafanyakazi wa Uhuru Media Group kwa mwaka huu wa 2018 wamefanya kazi kwa bidii, hivyo ameamua kuwapongeza kwa kuwapa motisha kwani kesho ni Januari moja ni vema wakauanza mwaka vizuri.
Kila mfanyakazi aliyeajiriwa na wasioajiriwa lakini wanafanya kazi kwenye vyombo vya habari vya chama tutawapa motisha hiyo. Tutafanya kwa walioko Dar es Salaam na wa mikoani," amesisitiza.
Amema, Mbali ya kutoa motisha atatumia nafasi hiyo kufanya uhakiki wa wafanyakazi waliopo kwenye vyombo hivyo na iwapo kutakuwa na wafanyakazi hewa atawabaini."Nataka kumuona kila mfanyakazi uso kwa uso.
Rais wetu aliamua kufanya uhakiki kwa watumishi wa Serikali ,nami namuunga mkono kwa kufanya uhakiki wa wafanyakazi wetu." amesema Sungura.
Amesema baada ya uhakiki wa majina, hatua ya pili itakuwa ni uhakiki wa vyeti vyao vya kitaaluma na mwisho wa siku atatoa taarifa lakini ameeleza nia yake ni kuona wote ambao wanalipwa wawe ni wafanyakazi sahihi na wapo kwenye orodha yake.
Kuhusu mipango yao, amesema kuanzia mwakani wataanza kufanya utafiti utakaochukua muda wa miezi mitatu na lengo ni kufahamu wasomaji wao, wasikilizaji wao na watazamaji wao wanataka nini.
Pia Februari mwaka 2019 watafanya 'uzinduzi laini' wa vyombo vyao na Aprili 2019 watafanya uzinduzi rasmi na hapo ndio watazungumza malengo na mikakati yao.
Amesema wanao mkakati wa kibiashara wa miaka minne na mkakati wa miaka 10 kwa ajili ya kulishika soko.
Pia watajiimarisha kwenye mitandao ya kijamii ili kuhakikisha wanawafikia wasomaji wengi zaidi kwani utafiti unaonesha nusu ya watu wote duniani wanapata habari kutoka mtandaoni
"Hivyo ili mambo yaende lazima mtandaoni nako tujiimarishe na mapema mwakani tutaweka nguvu kubwa katika eneo la mtandaoni kwa kuwa na timu maaluma," amesema.
Ametumia nafasi hiyo pia kuwatakia heri ya mwaka mpya wafanyakazi wote wa Uhuru Media Group huku akiwasisitiza waendelee kufanya kazi kwa bidii na kujituma kama ambavyo wamefanya mwaka 2018.
MKURUGENZI Mtendaji Mkuu wa Uhuru Media Group Ernest Sungura akimkabidhi mmoja wa wafanyakazi kutoka Idara ya Utawala,Banga Lucas kiasi cha fedha ikiwa ni sehemu ya motisha iliyotolewa kwa wafanyakazi wote wa kampuni hiyo ikiwa kama sehemu ya kuthamini mchango wao.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇