LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Dec 29, 2018

UCHAGUZI MKUU WA KONGO NA CHANGAMOTO

Uchaguzi mkuu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hatimaye utafanyika kesho Jumapili baada ya kuakhirishwa mara kadhaa. Raia wa nchi hiyo kesho Jumapili tarehe 30 Disemba wataelekea kwenye masanduku ya kupigia kura kumchagua mrithi wa Rais Joseph Kabila licha ya kuendelea mivutano ya kisiasa nchini humo.
Uchaguzi huo wa Rais na Bunge utafanyika kesho Jumapili huko Kongo huku nchi hiyo ikiendelea kusumbuliwa na  mgogoro wa kisiasa kwa miaka kadhaa sasa kutokana na kuakhirishwa mara kadhaa na kushindwa kufanyika uchaguzi mkuu kama ilivyokuwa inapangwa. Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo aliingia madarakani mwaka 2001 baada ya kuuawa baba yake, Laurent Desire Kabila, Rais wa wakati huo wa Kongo. Joseph Kabila ambaye amekuwa madarakani kwa mihula miwili, haruhusiwi kugombea tena kiti cha urais kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo. Kwa msingi huo uchaguzi mkuu umeakhirishwa mara kadhaa kwa visingizio mbalimbali.   
Uchaguzi huo wa kesho utafanyika baada ya makubaliano yaliyosainiwa mwaka jana kwa lengo la kuhitimisha mapigano huko Kongo. Chama tawala kimemuarifisha Emmanuel Ramazani Shadary, aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani na Katibu wa Kudumu wa chama tawala kuwa mgombea wa kiti cha urais katika uchaguzi wa kesho. 
Emmanuel Ramazan Shadary, mgombea wa kiti cha urais kwa tiketi ya chama tawala
Japokuwa vyama mbalimbali vya upinzani vimearifisha wagombea wao katika kinyang'anyiro hicho cha kesho, lakini mgombea mkuu wa wapinzani katika uchaguzi wa rais ni Martin Fayulu. Pamoja na hayo, wapinzani na wananchi wa Kongo wangali wana wasiwasi kuhusu uchaguzi huo wa kesho. Kufanyika zoezi hilo kwa njia ya kielektroniki kimewatia wapinzani wasiwasi kwamba, kuna uwezekano uchaguzi huo ukagubikwa na udanganyifu na uchakachuaji wa kura. Hatua ya serikali ya Kinshasa ya kuamiliana kwa mabavu na wapinzani, kuchomwa moto ghala la kuhifadhia vifaa vya uchaguzi la Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo ambapo vifaa vingi vya uchaguzi vimeteketea, na kuzuiwa uchaguzi katika miji mitatu ya Beni, Butembo na Yumbi ambayo ni ngome kuu za wapinzani, vimezidisha wasiwasi  kuhusu matokeo ya zoezi hilo. Pamoja na hayo, Rais Joseph Kabila ameahidi kuwa uchaguzi wa kesho Jumapili utakuwa huru na wa haki. 
Kuhusiana na suala hilo Rais Kabila wa Kongo anaeleza kuwa: Uchaguzi utafanyika vizuri sana. Huu utakuwa uchaguzi bora zaidi kuwahi kufanyika nchini tangu mwaka 1959.   
Uchaguzi mkuu wa kesho katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unafanyika huku nchi hiyo ikisumbuliwa na matatizo chungu nzima. Ugonjwa wa homa ya Ebola ulioyaathiri baadhi ya maeneo ya nchi hiyo hadi sasa umeua mamia ya watu na kuwaacha mamilioni ya wengine katika hatari ya kuambukizwa maradhi hayo. Licha ya kuwa hadi sasa kumefanyika mikakati mbalimbali ili kudhibiti maambukizi ya maradhi hayo hatari kwa msaada wa taasisi za kimataifa, lakini mapigano ya silaha, machafuko na mizozo ya kikabila bado vinatoa changamoto kubwa katika maeneo ya mashariki mwa Kongo. 
Charlie Yaxley Msemaji wa Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa ameashiria namna hali ya kutokuwa na makazi na mahali pa kuishi, ukosefu wa chakula cha kutosha na wimbi la wakimbizi linavyoongezeka katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo  na kueleza kuwa: Mlipuko wa ugonjwa hatari wa Ebola pia unatishia afya na maisha ya wakazi wa mikoa ya mashariki mwa Kongo mbali na maafa yanayosababishwa na mizozo ya silaha, machafuko na mapigano ya kikabila.  
Uchaguzi wa kesho katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo una umuhimu mkubwa sana kwa mustakbali wa kisiasa wa nchi hiyo na Wakongo, nchi jirani na jamii ya kimataifa kwa ujumla zinatarajia kwamba, utasahilisha zoezi la kwanza kabisa la kupokezana madaraka kwa njia ya amani nchini humo tangu mwaka 1960.  

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages