Serikali ya Sudan Kusini imepuuza vitisho vilivyotolewa na Marekani kwamba itakata misaada yake yote ya kifedha kwa nchi hiyo na kusisitiza kuwa havina maana.
Taarifa ya serikali ya Sudan Kusini iliyotolewa kujibu vitisho vya Marekani imesema kuwa, nchi hiyo haiongozwi kwa misaada ya kifedha ya Marekani.
Alkhamisi iliyopita serikali ya Marekani ilitishia kuwa, haitaipatia Sudan Kusini mkopo au misaada ya kifedha.
Uamuzi huo ulitangazwa na Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani, John Bolton akitangaza stratijia mpya ya serikali ya Donald Tramp. Marekani pia imetangaza vikwazo dhidi ya Wasudan Kusini watatu ambao inadai wana mchango katika vita vya ndani vya nchi hiyo.
Mwanzoni mwa mwaka huu wa 2018 pia Marekani ilishinikiza vikwazo vya silaha katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya serikali ya Sudan Kusini.
Vikwazo vya sasa vya Marekani dhidi ya Sudan Kusini vimewekwa baada ya serikali ya nchi hiyo na waasi kutia saini makubaliano ya amani mjini Addis Ababa hapo tarehe 5 Septemba.
Sudan Kusini ilitumbukia katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2013 baina ya jeshi la taifa linalomuunga mkono Rais Salva Kiir wa nchi hiyo na waasi wanaoongozwa na makamu wa zamani wa rais, Riek Machar.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇