Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameyataja matokeo ya awali ya mazungumzo ya amani ya Yemen huko Stockholm nchini Sweden kuwa chanya na yenye kuleta matumaini.
Akizungumza hayo jana Alkhamisi, Bahram Qassemi ameashiria mapatano yaliyofikiwa baina ya pande mbili nchini Yemen baada ya mazungumzo yaliyohusu mji na bandari ya Al Hudaydah na kuyataja kuwa muhimu sana.
Ameongeza kuwa mapatano hayo yanaonyesha kuwa, pande mbili katika mazungumzo hayo zimediriki hali mbaya waliyo nayo hivi sasa watu waliodhulumiwa Yemen. Amesema pande mbili katika mazungumzo hayo zimeamua kuacha maslahi binafsi kwa lengo la kuwaondolea masaibu Wayemen.
Qassemi aidha amebainisha matumaini yake kuwa, mapatano yaliyofikiwa Sweden yatatekelezwa kama ilivyopanga ili kuandaa mazingira ya duru nyingine ya mazungumzo ya kaundi ya Wayemeni kwa shabaha ya kufikiwa mapatano ya mwisho ya amani. Aidha ameongeza kuwa, "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika fremu ya sera zake za uwajibikaji kuhusu migogoro imekuwa na nafasi amilifu katika utekeelzwaji wa mapatano ya makundi ya Wayemen wenyewe kwa wenyewe ya huko nchini Sweden." Qassemi amesema utatuzi wa mgogoro wa Yemen na kuhitimishwa vita nchini humo kutawezekana tu kupitia mazungumzo ya Wayemen wenyewe kwa wenyewe.
Jana , Mohammad Abul Salam, kiongozi wa ujumbe wa Harakati ya Ansarullah katika mazungumzo ya Sweden alitangaza kuwa pande mbili zimeafikiana kuhusu usutishwaji mapigano katika bandari ya Al Hudaydah. Mazungumzo hayo yalianza Disemba sita na kumalizika Desemba 13 nchini Sweden. Utawala wa zamani wa Yemen unaoungwa mkono kikamilifu na Saudia ndio uliokuwa upande ya pili katika mazungumzo hayo yaliyofanyika chini ya upatanishi wa Umoja wa Mataifa.
Saudia ilianzisha mashambulio ya kijeshi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kumrejesha madarakani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kutoroka nchi.
Hata hivyo Saudi Arabia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao hayo huku wakisababisha maafa makubwa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na kuwaua raia wasiopungua 15,000 wasio na hatia.
Hujuma ya kijeshi ya Saudi Arabia imeifanya Yemen ikumbwe na matatizo mengi yakiwemo ya ukosefu wa huduma muhimu kama chakula na dawa huku asilimia kubwa ya miundombinu ya nchi hiyo ikiwa imeharibiwa vibaya na mashambulio hayo ya kikatili ya Saudia na wavamizi wenzake.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇