Erdogan: Muuaji wa Khashoggi alisikika akisema 'Najua Namna ya Kukata'
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amefichua kuwa katika sehemu ya faili la sauti kuhusu mauaji ya Jamal Khashoggi, mmoja kati ya wauaji wa mpinzani huyo wa utawala wa Saudia alisikika akijigamba kuwa, 'Najua namna ya kukata.'
Akizungumza Istanbul Ijumaa, Erdogan aliongeza kuwa tayari serikali ya Uturuki imeshakabidhi faili hilo la sauti kwa serikali za Marekani, Ujerumani, Ufaransa na Canada. Erdogan amesema muuaji huyo aliyejigamba anajua kukata ni mwanajeshi na kwamba mauaji hayo yalirekodiwa.
Jamal Khashoggi, aliyewahi kuwa msiri na mwandani wa aila ya kifalme inayotawala nchini Saudi Arabia, lakini hatimaye akageuka kuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Aal Saud, aliuliwa na mwili wake kukatwa vipande vipande, alipoingia kwenye jengo la ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul, Uturuki mnamo tarehe Pili Oktoba ili kukabidhi hati zake kwa ajili ya mpango wake wa kufunga ndoa. Katika faili hilo la sauti, baadaye ilisikika sauti ya msumeno ukikeketa na kuukata mwili wa mwandishi huyo.
Hivi karibuni pia vyombo vya habari vya Uturuki vilifichua kuwa, maneno ya mwisho yaliyotamkwa na mwandishi habari wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi yalikuwa ‘siwezi kupumua’.
Saudia imekataa ombi la Rais Erdogan la kuwakabidhi watuhumiwa wa mauaji ya Khashoggi wakashitakiwe nchini Uturuki.
Hivi karibuni pia ilibainika kuwa shirika moja la ujasusi wa intaneti la utawala wa Kizayuni wa Israel lilitoa msaada mkubwa kwa ufalme Saudi Arabia ili kufanikisha mauaji ya Khashoggi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇