NA TIGANYA VINCENT-RS TABORA
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Jukwaa la Biashara na Uwekezaji na Maonesho ya wajasiliamali mkoani Tabora.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati wa sala na dua maalumu ya kuliombea Jukwaa hilo iliyofanyika katika sanamu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Alisema Jukwaa hilo linatarajiwa kufunguliwa tarehe 21 Novemba mwaka huu na Waziri Mkuu Mheshimiwa Majaliwa na kufuatiliwa na uwaslishaji wa mada mbalimbali.
Mwanri alisema wakati wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kutakuwepo na mada mbalimbali za kutangaza fursa za biashara na uwekezaji zilizipo katika Halmashauri nane ya Mkoa wa Tabora zitawasilishwa na wadau mbalimbali.
Alisema kila Halmashauri mkoani humo imechagua maeneo muhimu ya uwekezaji ambayo itatumia fursa kuwatangazia wadau kwa ajili ya kuwavutia watu au Kampuni ambazo zinataka kuwekeza.
Mwanri aliwakaribisha wananchi wa mkoa huo na Watanzania wote kwa ujumla kuja kushiriki maonesho na Jukwaa hilo chini ya kauli mbiu ya wekeza Tabora kwa Mapinduzi ya Uchumi wa Kati.Mkuu huyo wa Mkoa aliongeza kuwa Jukwaa hilo pia litahudhuriwa na viongozi mbalimbali na Mawaziri. Jukwaa la Biashara na Uwekezaji limeandaliwa na Ofisi ya Mkoa wa Tabora na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) kwa lengo la kutangaza fursa za biashara na uwekezaji zinazopatikana mkoani humo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇