Na Jacquiline Mrisho, Dodoma.
Serikali imejipanga kuongeza kasi ya ukuaji wa Pato halisi la Taifa kufikia asilimia 7.3 mwaka 2019 ikiwa ni moja ya shabaha na malengo ya uchumi jumla.
Takwimu hizo zimetolewa leo jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango wakati akiwasilisha Bungeni Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Mwaka 2019/20.
Waziri Dkt. Mpango amesema kuwa katika robo ya kwanza ya mwaka 2018, Pato halisi la Taifa lilikua kwa asilimia 8.4 ikilinganishwa na asilimia 5.7 katika kipindi kama hicho mwaka 2017 ambapo shughuli za kiuchumi zilizokua kwa kiwango kikubwa ni ujenzi, habari na mawasiliano, usafirishaji na uhifadhi mizigo pamoja na kilimo.
"Serikali yetu imejipanga kuongeza kasi ya ukuaji wa Pato Halisi la Taifa kufikia asilimia 7.3 kwa mwaka 2019 ikilinganishwa na matarajio ya asilimia 7.2 mwaka 2018 na kuongezeka kwa wastani wa asilimia 7.6 katika kipindi cha muda wa kati (2019/20 - 2021/22)", alisema Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango ametaja shabaha na malengo mengine ya uchumi, yakiwemo ya kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja ya wastani wa asilimia 5 katika kipindi cha muda wa kati pamoja na mapato ya kodi kufikia asilimia 12.7 ya Pato la Taifa mwaka 2019/20 kutoka matarajio ya asilimia 12.5 mwaka 2018/19.
Vile vile, Serikali imejipanga kupunguza nakisi ya Bajeti kutoka matarajio ya asilimia 2.9 mwaka 2018/19 hadi wastani wa asilimia 1.1 katika kipindi cha muda wa kati pamoja na kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi 4.5.
Akiwasilisha hoja hiyo, Waziri Mpango amefafanua kuwa misingi iliyozingatiwa katika kuweka malengo ya uchumi jumla ni pamoja na uwepo wa amani, usalama, utulivu na umoja wa nchi na nchi jirani, kuimarika kwa viashiria vya uchumi jumla, kutengamaa kwa uchumi wa dunia, utulivu wa bei za mafuta katika soko la dunia na hali nzuri ya hewa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, George Simbachawene amesema kuwa kuna baadhi ya miradi ya maendeleo ambayo iliainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2018/19 lakini haionekani katika mapendekezo ya Mpango wa Mwaka 2019/20 hivyo kamati imeshauri miradi hiyo ijumuishwe katika Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2019/20.
Aidha ametoa rai kwa Serikali kuanza kutenga kiwango cha asilimia moja ya Pato la Taifa kwa ajili ya shughuli za utafiti na maendeleo.
Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Mwita Mwikabe Waitara (CCM), akila kiapo mbele ya Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai wakati wa kikao cha kwanza Bunge la 13 leo jijini Dodoma. Wabunge wanne wameapishwa baada ya kuchagulia kutokana na kuhama vyama vyao. Wabunge hao ni Julias Kallanga (Monduli – CCM), Mhe. Kuchauka (Liwale – CCM), pamoja na Thimotheo Mnsava ( Korogwe Vijijini –CCM) aliyechukua nafasi ya Stevene Ngonyani (Majimarefu aliyetangulia mbele za haki). Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimskiliza kwa makini Waziri wa Ardhi Nyumba na Maenddeleo ya Makzi, William Lukuvi (kushoto) wakati wa kikao cha kwanza cha Mkutano wa 13 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo jijini Dodoma.
Kutoka kushoto ni Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Phillip Mpango, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga wakifuatilia kitabu cha Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Mwaka 2019/2020 katika kikao cha kwanza cha Mkutano wa 13 wa Bunge la Jamhuri la Muungano leo jijini Dodoma. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) akiteta jambo na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Khamis Kigwangallah (kushoto) wakati wa kikao cha kwanza cha Mkutano wa 13 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo jijini Dodoma. Katikati ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Janeth Massaburi. Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde akijibu swali wakati wa kikao cha kwanza cha Mkutano wa 13 wa Bunge la Jamhuri la Muungano leo jijini Dodoma. Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile akifafanua jambo wakati wakati wa kikao cha kwanza cha Mkutano wa 13 wa Bunge la Jamhuri la Muungano leo jijini Dodoma. Kutoka kulia ni Waziri wa Mabo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Joseph Kandege. Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akijibu swali wakati wa kikao cha kwanza cha Mkutano wa 13 wa Bunge la Jamhuri la Muungano leo jijini Dodoma. Baadhi ya wageni wakifuatili kikao cha kwanza cha Mkutano wa 13 wa Bunge leo jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇