Rais John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Baraza la Maulid litakalofanyika wilayani Korogwe mkoani Tanga.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Jumanne Novemba 13, 2018, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zuberi amesema baraza hilo limeandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata).
Amesema Maulid hayo ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) yatafanyika Novemba 19.
Amewataka wananchi wa Tanga na mikoa jirani kuhakikisha wanafika kwenye maulidi hayo yanayofanyika mara moja kwa mwaka, huku akisema kuchaguliwa mkoa huo ni bahati hivyo wajitokeze kwa wingi.
Kiongozi huyo wa kiroho, amekemea vitendo vya mmomonyoko wa maadili nchini akisema hatua hiyo ndiyo chanzo cha vijana wengi kupiga picha za utupu bila aibu na kuziweka kwenye mitandao ya kijamii.
Amesema vitendo hivyo vinavunja hadhi ya nchi na kuomba waliofanya hivyo wakadhibitika sheria kali zichukuliwe dhidi yao ili angalau kukomesha hali hiyo inayotia doa taifa kwa ujumla.
''Hii inasababishwa na malezi mabaya nyumbani kwani mtu mwenye akili timamu hawezi kuvunja heshima yake kwa kuweka picha chafu za kwenye mitandao ya kijamii huo ni uvunjifu wa maadili kwa kiasi kikubwa,'' amesema
Alisema mengi yanayohusu kukemea tabia hiyo yataongelewa na watu maalum kwenye maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa baraza hilo hapa nchini ambalo lilianzishwa mwaka 1968 mpaka sasa.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇