LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 24, 2018

RAIS WA ZANZIBAR NA RAS AL KHAIMA WATILIANA SAINI MKATABA WA MGAWANYO WA UZALISHAJI WA MAFUTA NA GESI ASILIA


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohammed Shein, (kulia), akiwa na mgeni wake, Shaikh Saud Bin Saqr Al Qasimi, Mtawala wa Ras Al Khaimah, katika hafla ya Utiaji Saini Mkataba wa Mgawanyo wa Uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia, hafla iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu mjini Zanzibar Oktoba 23, 2018
NA MWANDISHI MAALUM, ZANZIBAR


MALENGO ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuhakikisha kuwa faida zitakazopatikana kutokana na rasilimali ya mafuta na gesi asilia zinachangia katika ukuaji wa uchumi na zinawanufaisha wananchi wote bila ya kuwatenga na kuwabagua wengine. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameyasema hayo Oktoba 23, 2018 katika viwanja vya Ikulu Mjini Zanzibar katika hafla ya Utiaji Saini Mkataba wa Mgawanyo wa Uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia, hafla iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu mjini Zanzibar ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na viongozi kutoka Ras al Khaimah. Katika hafla hiyo ambayo mapema Rais Dk. Shein na mgeni wake Shaikh Saud Bin Saqr Al Qasimi, Mtawala wa Ras Al Khaimah walishuhudia utiaji saini wa Mkataba huo, aliwahimiza wananchi waendelee kushirikiana na kuimarisha umoja na mshikamano ili kuweza kupata mafanikio yanayotarajiwa. Dk. Shein alisema kuwa suala la utafutaji wa mafuta na gesi asilia ni jambo linalohusu maendeleo ya Zanzibar na kamwe halitakiwi lilete mfarakano katika jamii na badala yake linatakiwa liwaunganishe wananchi. Aliwataka wananchi kujiepusha na watu wachache ambao wameamua kulitumia jambo hilo kuwa ajenda ya kuwagawa watu jambo ambalo ni kinyume na malengo ya Serikali ya kuzishughulikia rasilimali hizo. Aidha, Rais Dk. Shein aliendelea kuwahimiza wananchi wa Zanzibar wawe na subira kwa kutambua kwamba suala la utafutaji wa mafuta na gesi asilia ni kazi inayochukua muda mrefu. 


Rais Dk. Shein alitoa shukurani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli kwa kushirikiana nae vyema pamoja na mashirikiano mazuri yaliopo baina ya Serikali zao mbili hatua ambayo imepelekea Mkataba huo umeweza kutiwa saini. Dk. Shein alitoa shukurani kwa Mtawala wa Ras Al Khaimah Shaikh Saud Bin Saqr Al Qasimi pamoja na ujumbe aliofuatana nao kwa kujumuika pamoja katika hafla hiyo huku akitoa shukurani maalum kwa viongozi wa Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa kushirikiana kwa kufanya kazi pamoja kwa lengo la kuimarisha sekta za kiuchumi na kijamii. Alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kwa hatua alizozichukua ili kuhakikisha kuwa kabla ya kustaafu kwake suala hilo linapatiwa ufunbuzi na kuondoa kero ya muda mrefu. Rais Dk. Shein alisema kuwa tukio la utiaji saini Mkataba wa Mgawanyo wa Uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia linathibitisha jinsi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba inavyotekeleza kwa mafanikio Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM, Sera zake na ahadi ambazo ziliahidiwa wakati wa kampeni mwaka 2015. Aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inajivunia hatua hiyo muhimu kwa maendeleo na utekelezaji wa dhamira ya kuiendeleza sekta ya Mafuta na Gesi Asili hapa Zanzibar. Alisema kuwa Mkataba huo uliotiwa saini unahusisha kitalu cha Pemba-Zanzibar tu ambacho kinajumuisha maeneo yaliyopo nchi kavu na baharini hivyo, viko vitalu ambavyo havimo katika makubaliano hayo yaliosainiwa. Alisema kuwa kuimarika kwa uchumi ni kunawiri kwa hali na maisha ya watu wa Zanzibar hali ambayo itapelekea kuongezeka kwa Pato la Taifa na Pato la kila mwananchi jambo ambalo litanyanyua hali ya maisha yao ya kila siku. Nae Mtawala wa Ras Al Khaimah Shaikh Saud Bin Saqr Al Qasimi akitoa salamu zake kwa wananchi wa Zanzibar alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa jinsi anavyowapenda watu wa Zanzibar ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wake na watu kwa kufanikisha jambo hilo kwa haraka. Aidha, alisisitiza kuwa Ras al Khaimah pamoja na nchi zote za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) wana uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu kwa nchi za Afrika ya Mashariki ikiwemo Tanzania ambapo kwa Zanzibar wana uhusiano maalum.




No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages