Waziri wa nchi OR-TAMISEMI Mhe.Seleman Jafo ameipongeza Manispaa ya Ilemela kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo inayozingatia thamani ya fedha.
Pongezi hizo amezitoa akiwa kwenye ziara ya kikazi katika Manispaa ya Ilemela kwa ajili ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo alikagua jengo la utawala la Halmashauri, jengo la hospitali ya Wilaya, ujenzi wa barabara ya Sabasaba-Kiseke-Buswelu pamoja na ujenzi wa miundombinu katika kituo cha Afya Buzuruga.
Sanjari na ukaguzi wa miradi hiyo aliongea na watumishi wa Manispaa na kuwasisitiza kufanya kazi kwa ueledi na kujiamini huku akisisitiza suala la ukusanyaji wa mapato na kumtaka Mstahiki Meya wa Manispaa kuhakikisha anasimamia ipasavyo ukusanyaji wa mapato hasa katika soko la samaki la Mwaloni kwani ndio chanzo kikuu cha mapato cha Halmahauri.
“Mna kila sababu ya kusimamia mapato katika soko la samaki,hakikisheni mapato yote ya soko yanaingia vizuri na yanasimamiwa vizuri, sitaki kusikia soko la mwaloni linaharibiwa kuwa sio chanzo muhimu cha mapato ya Manispaa ya Ilemela”, Alisisitiza
Aidha amemtaka afisa mapato kuhakikisha anasimamia mapato na kama kuna wizi unaendelea basi ahakikishe anafunga mianya yote hasa katika soko la samaki na kuongeza kuwa anataka kuona mapato yanaongezeka na halmashauri inasonga mbele
Pia amewapongeza waheshimiwa madiwani kwa usimamizi wao mzuri na kuwataka kuendelea kupambana katika kuisimamia manispaa pamoja na miradi ya maendeleo ili Manispaa iweze kusonga mbele
Akiwa katika kituo cha Afya Buzuruga, ambapo alipata wasaa wa kuongea na wagonjwa waliofika kutibiwa, Mhe. Jafo amesema kuwa amefarijika kuona kuwa Manispaa ya Ilemela imefunga mifumo ya kielektroniki (GOTHOMIS) katika vituo vyote vya afya na zahanati na kuifanya Halmashauri hii kuwa ya kwanza ya mfano na hivyo ameziagiza Halmashauri zote kukamilisha uwekaji wa mifumo ya hii.
Pamoja na hayo ameitaka Halmashauri kuhakikisha wanaitumia mifumo hiyo kwa lengo lililokusudiwa la ukusanyaji wa mapato kwa maslahi mapana ya Halmashauri na vituo vya afya huku akiwasisitiza watumishi kufanya kazi kwa ueledi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇