Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM kimetangaza habari ya kufanikiwa kumuangamiza Mdhibiti Mkuu wa Fedha wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la al-Shabaab.
AMISOM imeandika katika ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa, kamanda huyo mwandamizi wa masuala ya fedha za al-Shabaab ameuawa katika mji wa Bariire, yapata kilomita 60 kusini mwa mji mkuu Mogadishu, baada ya wanajeshi wa kikosi hicho cha kieneo kuvamia mkutano wa makamanda wa genge hilo la kitakfiri.
Kikosi cha AMISOM bila kutaja jina, uraia wala utambilisho wake kimesema kuwa, kamanda huyo wa al-Shabaab aliyeua alikuwa mkuu wa ukusanyaji kodi wa kundi hilo la kigaidi, katika eneo la Lower Shabelle.
Taarifa ya Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia imeongeza kuwa, siku moja kabla ya kuuawa Mdhibiti Mkuu wa Fedha za al-Shabaab, wanachama wengine sita wa kundi hilo waliuawa katika operesheni nyingine ya AMISOM.
Somalia ilitumbukia katika mapigano na machafuko ya ndani tangu ilipoondolewa madarakani serikali ya Mohamed Siad Barre mwanzoni mwa muongo wa 1990. Mbali na harakati za kundi la kigaidi la al-Shabab kuwa tatizo kuu nchini Somalia, nchi hiyo inakabiliwa pia na ukame na baa la njaa.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇