LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 10, 2018

KIKAO CHA KWANZA CHA BARAZA LA WADHAMINI LA CCM


CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)

TAARIFA KWA UMMA

KIKAO CHA BARAZA LA WADHAMINI LA
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)
_______________

Ofisi Ndogo ya Makao Makuu, Lumumba
10 Oktoba 2018

Baraza la Wadhamini wa Chama Cha Mapinduzi, chini ya Mwenyekiti wake Mama Anna Magreth Abdalla limekutana kwa mara ya kwanza tangu kuteuliwa kwake tarehe 10/07/2018. Kikao hicho kilichofanyika kuanzia tarehe 08 hadi 10 Oktoba 2018 Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya Chama Lumumba, Dar es Salaam. Katika kikao hicho, pamoja na mambo mengine, Baraza limeipitia kwa kina na kuanza kuifanyia kazi Ripoti ya Tume ya Kuhakiki Mali za Chama na Jumuiya zake, kwa lengo la kuchambua na kuzifanyia kazi changamoto na Mapendekezo yote ya Tume yanayohusiana na Mali za CCM.

Kwa mujibu wa ibara ya 125 ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977, Toleo la 2017, BARAZA LA WADHAMINI WA CCM, ndilo lenye jukumu la kumiliki na kusimamia Mali zote (mali zinazoondosheka na zisizoondosheka) za CCM na Jumuiya zake.  Hivyo, baada ya kupitia taarifa hiyo kwa umakini, Baraza limeona ni vema kutoa taarifa kwa umma wa wanachama na wananchi juu ya masuala yafuatayo:-

1.        Baraza linawataka watendaji na viongozi wote wa Chama na Jumuiya zake wa ngazi mbalimbali kuhakikisha kwamba, katika maeneo yao hakuna mali yoyote ya CCM au Jumuiya zake inayouzwa, kukodishwa, kumilikishwa au kuhaulishwa kwa mtu yeyote au chombo kingine BILA IDHINI yaBARAZA LA WADHAMINI WA CCM.

2.        Baraza limebaini kuwa pamoja na uwepo wa mikataba isiyo na tija, kuna uuzaji, uporaji na uvamizi wa mali za Chama kinyume na katiba ya CCM, hivyo Baraza linatoa ONYO KALI kwa watendaji na viongozi wote wa CCM na Jumuiya zake, kuacha mara moja tabia hiyo.

3.        Baraza linaagiza na kuzitaka Mamlaka zote husika za Chama na Jumuiya zake, kutowafumbia macho na kuwachukulia hatua kali za Kinidhamu Watendaji na Viongozi wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya uuzaji wa mali za CCM au Jumuiya zake bila kibali cha BARAZA LA WADHAMINI.

4.        Baraza limebaini kuwa Rasilimali ardhi nyingi za Chama hazina hati miliki, hivyo linawaagiza Watendaji na Viongozi wote katika ngazi mbalimbali za Chama na Jumuiya zake kukamilisha mchakato wa kupata Hati miliki  ndani ya kipindi kisichozidi mwaka mmoja kuanzia leo tarehe 10/10/2018.

5.        Baraza linawatahadharisha wanachama na wananchi wote kuwa ni kosa kununua maeneo ya Chama na Jumuiya zake bila kibali cha BARAZA LA WADHAMINI WA CCM.

6.        Baraza linawashukuru wanachama na wananchi wenye mapenzi mema na Chama kwa kutoa taarifa ya Mali za Chama na Jumuiya zake, na pia linawaomba waendelee kutoa taarifa ya Mali za Chama na Jumuiya zake zilizouzwa, zilizofichwa, zilizoporwa au kuhaulishwa kinyume cha Katiba ya Chama Cha Mapinduzi.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

Ndg. Anna Magreth Abdalla
MWENYEKITI

BARAZA LA WADHAMINI WA CCM  

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages