LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 26, 2018

ERDOGAN AITAKA SAUDIA IMFICHUE ALIYETOA AGIZO LA KUUA JAMAL KHASHOGGI

Kwa mara nyingine tena Rais Recep Tayyib Erdogan wa Uturuki ameitaka Saudi Arabia imfichue mtu ambaye alitoa amri ya kuuawa Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari na mkosoaji mkubwa wa utawala wa Aal-Saud.
Erdogan amekariri hayo leo akihutubia wanachama wa chama chake tawala cha Justice and Development Party (AKP) mjini Ankara na kuongeza kuwa, Riyadh inapaswa kuweka wazi jina la mtu aliyewapa agizo watu 15 walioenda Istanbul kufanya mauaji hayo.
Rais wa Uturuki amehoji, "kwa nini raia hao 15 wa Saudia walikutana Istanbul? Nani aliwapa maagizo hayo? Kwa nini ubalozi mdogo wa Istanbul haukufunguliwa mara moja baada ya kuuawa Khashoggi bali siku kadhaa baadaye?
Kadhalika ameitaka Saudia ifichue uliko mwili wa Khashoggi sanjari na kumfichua raia wa Uturuki ambaye Riyadh inadai ilimkabidhi mwili wa Khashoggi baada ya kuuawa. Rais Erdogan wa Uturuki amesema Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Saudia anatazamiwa kukutana na mwenzake wa Uturuki mjini Istanbul siku ya Jumapili.
Jamal Khashoggi
Itakumbukwa kuwa, Erdogan wakati akihutubia wabunge wa chama tawala katika Bunge la nchi hiyo Jumanne iliyopita alisema mauaji hayo yalipangwa siku nyingi kabla ya kutekelezwa, na kwamba wahusika wanapashwa kubebeshwa dhima na kesi zao zinafaa kusikilizwa mjini Istanbul. 
Jamal Khashoggi aliyekuwa mwandishi katika gazeti la Washington Post na mkosoaji wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia aliuawa tarehe Pili mwezi huu wa Oktoba ndani ya ubalozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul nchini Uturuki. 

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages