Wabunge wa maeneo yote yanayozalisha kahawa
nchini wakifatilia taarifa iliyowasilishwa na Mhe
Mhandisi Dkt Charles Tizeba, Waziri wa kilimo mbele ya Dkt Bashiru Ali Kakurwa
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Tarehe 14 Septemba 2018 kwenye ukumbi wa White House
Mjini Dodoma.
Dkt Bashiru Ali Kakurwa Katibu Mkuu wa Chama
Cha Mapinduzi akizungumza mara baada ya Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba, Waziri
wa kilimo kutoa ufafanuzi kuhusu zao la kahawa wakati akiwasilisha taarifa ya
mwenendo wa soko la kahawa nchini, Tarehe 14 Septemba 2018 katika ukumbi wa
Chama Cha Mapinduzi maarufu White House Mjini Dodoma.
Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba, Waziri wa
kilimo akitoa ufafanuzi kuhusu zao la kahawa wakati akiwasilisha taarifa ya
mwenendo wa soko la kahawa nchini kwa Dkt Bashiru Ali Kakurwa Katibu Mkuu wa
Chama Cha Mapinduzi mkutano uliohudhuriwa na wabunge kutoka maeneo yote
yanayozalisha kahawa, Tarehe 14 Septemba 2018 katika ukumbi wa Chama Cha
Mapinduzi maarufu White House Mjini Dodoma.
Na
Mathias Canal-WK, Dodoma
Ushirika ni dhana ya kuleta
maendeleo kwa kushirikiana, Dhana hii imetajwa kuwa imefanikiwa kuleta
mabadiliko ya kiuchumi na kijamii katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita,
Kutokana na changamoto mbalimbali zilizoikumba sekta hii ya ushirika watu wengi
walikosa imani na vyama hivyo kutokana na viongozi wake kutokuwa waaminifu
(Wabadhilifu).
Hayo yalibainishwa juzi tarehe
14 Septemba 2018 na wabunge kutoka maeneo yote yanayozalisha kahawa nchini
hususani katika mikoa ya Kagera, Mara, Kilimanjaro, Mbeya, Arusha, na Manyara
wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya mwenendo wa soko la kahawa nchini kwa Dkt
Bashiru Ali Kakurwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi katika ukumbi wa
mikutano wa CCM Makao makuu maarufu kama White House
“Mnyonge mnyongeni lakini haki
yake mpeni Ni wazi kuwa katika kipindi cha miaka miwili hivi tangu Mhandisi Mhe
Dkt Charles Tizeba, Waziri wa kilimo wakati kushika nafasi katika wizara hii
amefanya kazi kubwa mno, imani kwa vyama vya ushirika imeongezeka na vyama
vingi vinaendelea kuundwa hasa vile vya kuweka na kukopa, yaani SACCOS”
Walisema
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na
Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali Mstaafu Ngemela Lubinga,
Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa (NEC) Makongoro Nyerere,
Naibu waziri wa Kilimo, Mhe Omary Mgumba, wataalamu kutoka wizara ya kilimo
akiwemo Naibu katibu Mkuu Prof Sizya Tumbo, Mrajis wa vyama vya ushirika,vyama
vya ushirika na wawakilishi wa wakulima kutoka maeneo yanayolima kahawa.
Wabunge hao walitaja kuwa
ushirika ni sekta mtambuka inayohusisha sekta mbalimbali zikiwemo Kilimo,
Ufugaji, Uvuvi, Madini, Viwanda, Nyumba na Fedha (Ushirika wa Akiba, Mikopo na
Benki) ambazo zinagusa wananchi wengi zaidi hivyo kutokana na maelezo ya
kuridhisha yaliyotolewa na Dkt Tizeba katika taarifa yake ya mwenendo wa zao la
kahawa ni wazi kuwa yameridhiwa hivyo wabunge hao wameunga mkono na kuihubiri
dhana ya ushirika kwa asilimia 100%.
Katika taarifa hiyo Waziri wa
kilimo Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba alisisitiza kuwa kutokana na umuhimu wa
sekta hiyo, Wizara kupitia Tume ya maendeleo ya ushirika imeendelea kuwezesha
na kuimarisha ushirika ili wananchi waweze kunufaika na fursa zinazopatikana
katika ushirika kwa lengo la kuchangia katika kuongeza kipato kwa wananchi
wengi hususani waliopo vijijini.
Alisema katika mwaka 2017/2018, Tume
imefanya uhamasishaji wa wananchi kujiunga au kuanzisha vyama vya ushirika
ambapo hadi kufikia Disemba 2017 vyama vipya 394 vilisajiliwa na kufanya idadi
ya vyama vya ushirika kufikia 10,990 kutoka 10,596 vilivyokuwepo Machi 2017.
Alisema vyama hivyo vinakadiriwa
kutoa ajira mpya kwa wananchi takribani 1,182 huku katika kipindi cha mwaka
2017/2018 wanachama wapya 385,295 walijiunga au kuanzisha vyama vya ushirika na
kufanya idadi ya wanachama kuongezeka kutoka 2,234,016 hadi kufikia 2,619,311
Alisema kuwa uanzishwaji wa
vyama vingi vya ushirika kwa sasa unatokana na elimu watu wengi waliyoipata
kuhusu Ushirika na watu kuendelea kuelewa kuwa changamoto zilizoko ndani ya
ushirika zinatatulika ikiwa ni pamoja na hivi karibuni kutangaza kiama kwa baadhi
ya viongozi wabadhilifu wa vyama hivyo ambao wanautumia ushirika kama sehemu ya
kujinufaisha wao pasina kuwa na mtazamo wa mafanikio kwa wanachama wote.
Alisema, Dhamira ya Ushirika ni
nzuri na kama itafanya kazi vizuri ni njia nzuri ya kuleta mabadiliko kwa watu
wengi huku akisisitiza Wanachama wa Ushirika kujiimarisha katika misingi ya
uaminifu, uwazi, uwajibikaji kwa jamii na kuwajali wengine.
Dkt Tizeba alisema Ushirika ni
muungano wa watu ambao wanafanya kazi pamoja kwa hiari ili kufanikisha mahitaji
yao ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni kupitia shughuli ya biashara
inayomilikiwa kwa pamoja na kudhibitiwa kidemokrasia kwani njia pekee yenye
tija na mafanikio ya kilimo kwa mkulima ni kuuza mazao yao kupitia mfumo huo
rasmi wa ushirika.
“Kupitia ushirika kutamfanya mkulima kujihami na bei kwa kuuza kwa pamoja kwani
kwa muda mrefu kilimo cha masoko kimekuwa kikitengenezwa na wakulima wenyewekwa
sababu ya kutojiunga pamoja na kuwa na mfumo rasmi” Alikaririwa Dkt tizeba na
kuongeza kuwa
“Kunapokuwa na chama imara cha Msingi, chama hiki kinaunda chama kikuu kilicho
imara kwa kufanya hivyo tutaondokana na uduni wa bei kwa mkulima kutokana na
kushuka bei kwa mazao kwa sababu ya mkulima mmoja mmoja kuuza mazao yake
mwenyewe” Alisema
Waziri huyo wa kilimo Mhe Dkt. Charles Tizeba alisema Serikali imeamua kufufua
ushirika kwa sababu ndiyo mkombozi wa wakulima. "Tumeamua kurudisha
ushirika aminifu kwa wakulima, na nirudie kutoa onyo kwa viongozi waliopata
dhamana ya kuongoza ushirika wasidhani kule wameenda kupata ulaji.” Alisema
Kwa upande wake Dkt Bashiru Ali Kakurwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi
akizungumza mara baada ya mjadala huo kutuama kwa masaa 8 kujadili namna ya
kupata masoko ya mazao ya kilimo, urahisi wa upatikanaji wa mitaji, siasa ya
kilimo kupitia ushirika na maandalizi ya miundombinu rafiki katika kilimo,
alisema katika kipindi cha miaka mitano Chama Cha Mapinduzi kupitia ilani ya
ushindi ya mwaka 2015-2020 kimeweka kipaumbele cha kuhakikisha kuwa kilimo
nchini kinakuwa endelevu na chenye tija ili kuliwezesha Taifa kuwa na
utoshelevu wa chakula na kuongeza mapato ya wakulima na kuwa chanzo cha
kuaminika cha malighafi ya sekta ya viwanda.
Dkt Bashiru alinukuu ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020
katika sura ya pili ibara ya 22 inayosisitiza kuviimarisha na kuviwezesha vyama
vya ushirika kuwa na uwezo wa kutafuta masoko ya mazao ya wakulima ya ndani na
nje kwa kuweka mfumo madhubuti wa ukusanyaji, uchambuzi na uenezaji wa taarifa
za masoko na kutoa elimu juu ya uongezaji wa thamani na biashara.
Aidha, Dkt Bashiru alisimsisitiza Mrajis wa Vyama vya ushirika nchini kuongeza
ufanisi katika kuwajengea uwezo viongozi wote wa Vyama vya ushirika ili
kuongeza ufanisi na tija katika utendaji.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇