LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Sep 26, 2018

UTEKELEJI WA AGIZO LA WAZIRI LUGOLA KUFUNGA TELA BODABODA

Ikiwa imepita miezi miwili tangu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola kuagiza pikipiki zote zinazotumika kusafirisha abiria zifungwe tela katika kile kinachoaminika kudhibiti wimbi la ajali za bodaboda,Taasisi mbalimbali za Serikali zimekutana jijini Dodoma ikiwa ni mazungumzo ya awali kuelekea mkakati huo wa kupunguza ajali.

Akizungumza jijini Dodoma  baada ya mkutano  na ukaguzi wa pikipiki ya mfano iliyofungwa tela  iliyotengenezwa na Shirika la Mzinga,lililoko chini ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu, amesema Serikali imedhamiria kuondoa na kukomesha ajali za bodaboda pamoja na kulinda usalama wa watumiaji wa usafiri huo.

Akielzezea juu ya mazungumzo hayo yaliyokutanisha taasisi hizo, Katibu Mkuu Meja Jenerali Jacob Kingu, amesema Wizara yake kwa kushirikiana na wadau wengine kutoka taasisi za serikali; Shirika la Mzinga, Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (VETA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Kiwanda cha Kutengeneza Magari (NYUMBU) na Jeshi la Polisi watahakikisha wanakuwa na mpango wa pamoja wa kuratibu na kuhakikisha mkakati huo utakaosaidia kupunguza ajali unakamilika.

“Leo tumekutana hapa kujadili jinsi ya kuliendea jambo hili la kufunga tela na kamati ya  wataalamu hawa ndio itakutana na kuratibu andiko ambalo litapelekwa  kwa viongozi wa wizara mbalimbali zinazohusika na suala la kudhibiti ajali za barabarani na kumlinda mtumiaji wa huduma ya usafiri huo,” alisema Meja Jenerali Kingu.

Aliwaomba wananchi wawe na subira katika kipindi hiki ambacho kamati hiyo ya wataalamu inaenda kuandaa mpango huo, na mapema mwishoni mwa mwaka huu mpango huo utatangazwa .

Akizungumzia pikipiki hiyo ya mfano yenye tela, Mtaalamu kutoka Shirika la Mzinga, Mhandisi Salum Kipande alisema pikipiki hiyo wameitengeneza vizuri na itakua na uwezo wa kubeba abiria wanne na dereva mmoja huku akiahidi kuunga mkono adhma hiyo ya serikali kupunguza ajali za bodaboda nchini kwa kutengeneza pikipiki hizo kwa ustadi.

Naye Kaimu Mkurugenzi Elimu na Mafunzo wa Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (VETA), Stella Ndimubenya  alisema  wao kama VETA watahakikisha wanatumia teknolojia waliyonayo kuweka kifaa maalumu ambacho kitadhibiti upakiaji wa abiria kupita kiwango kilichopitishwa na mamlaka husika huku akiahidi kutoa mafunzo kwa madereva pindi pikipiki hizo zitakapopitishwa na kuanza kutumika.
Advertisement

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages