LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Sep 23, 2018

USAMBAZAJI WA PEMBEJEO ZA KILIMO UWAGUSE WAKULIMA WADOGO

  •  Na Ismail Ngayonga
    MAELEZO
    DAR ES SALAAM
    SERIKALI kupitia Wizara ya Kilimo inatekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) ambayo ni utekelezaji wa Mpango wa Uwekezaji katika Sekta ya Kilimo Nchini (TASFIP) unaolenga kukuza kilimo kwa asilimia 6 kwa mwaka.
    Kwa kuzingatia hatua hizo, Wizara ya Kilimo imekusudia kuleta mageuzi ya kilimo kutoka mtazamo uliopo wa kilimo cha kujikimu hadi kufikia uendeshaji wa kilimo kwa mfumo wa kibiashara.
    Aidha upatikanaji wa chakula cha kutosha unategemea kwa kiasi kikubwa ongezeko la uzalishaji katika sekta ya kilimo, hususan mazao ya nafaka, ambayo upatikanaji wake hupunguza gharama za maisha kwenye chakula.
    Inaelezwa kuwa asilimia 80 ya Watanzania wote wanaishi vijijini, kati yao wakulima wadogo wanakadiriwa kufikia Milioni 20 wanaopaswa kuguswa na mageuzi ya kiuchumi kama inavyoelezwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.
    Pamoja na Tanzania kuwa rasilimali za kutosha zinazoweza kusaidia kuleta mabadiliko ya uchumi na kuinua hali za maisha ya wananchi, sekta ya kilimo inaelezwa kukabiliwa na changamoto mbalimbali.
    Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na pembejeo zisizotosheleza kama vile mbegu bora, mbolea na dawa za kilimo, mfumo wa kizamani wa uoteshaji mazao na ucheleweshaji wa maendeleo ya miundombinu kama vile, skimu za umwagiliaji, miundombinu ya masoko.
    Katika mwaka 2015/2016 makadirio ya mahitaji ya pembejeo za kilimo nchini yalikuwa tani 485,000 za mbolea, tani 60,000 za mbegu bora, miche ya chai 1,700,000, miche ya kahawa 5,000,000, viuatilifu vya korosho tani 25,000 na viuatilifu vya pamba ekapaki 1,500,000.
    Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2018/19, Waziri wa Kilimo, Dkt Charles Tizeba anasema Serikali imeendeleamsukumo pia umewekwa katika kuimarisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo ikiwemo mbegu bora na Viuatilifu nchini.
    Anasema katika mwaka 2017/18 upatikanaji wa mbegu bora ulifikia tani 51,700.51 ikilinganishwa na tani 28,278.2 za mwaka 2016/2017, ambapo tani 26,112.69 zilizalishwa nchini na tani 16,277.7 ziliagizwa kutoka nje na wafanyabiashara.
    “2018/2019, Wizara itachangia upatikanaji wa tani 40,000 za mbegu bora mbalimbali; miche bora ya chai milioni 10 na miche bora ya kahawa milioni 12; kusambaza tani 8,600 na lita 9,800 za viuatilifu” anasema Waziri Tizeba.
    Dkt. Tizeba anasema Wizara kwa kushirikiana na Taasisi ya Bill and Melinda Gates Foundation itakamilisha Mfumo wa Taifa wa kuimarisha upatikanaji wa mbegu bora ikiwemo uboreshaji wa uzalishaji wa mbegu mama katika vituo vya utafiti pamoja na kujenga uwezo wa Taasisi ya Uthibiti wa Ubora wa Mbegu (TOSCI).
    Waziri Tizeba anasema Serikali kupitia Bodi ya Korosho Tanzania kwa kushirikiana na Vyama Vikuu vya Ushirika wa Korosho na Benki ya NMB imekamilisha mchakato wa uagizaji wa pembejeo za korosho ikiwemo kuingia mikataba na wazabuni ambao kwa ujumla wao wataleta salfa ya unga tani 35,000 na viuatilifu vya maji lita 520,000.
    Kilimo ni sekta muhimu katika maendeleo ya uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla hususani katika wakati huu tunapojidhatiti kufikia uchumi wa viwanda, ambapo asilimia 65 ya malighafi hutegemea mazao ya kilimo.
    Uamuzi wa Serikali wa kujenga uchumi wa Viwanda unalenga kuleta maendeleo jumuishi na endelevu kwa kutumia rasilimali zilizopo na hivyo kuchangia katika kukuza pato la taifa, kutoa nafasi za ajira na kuzalisha bidhaa bora kwa masoko ya ndani na nje ya nchi.
    Ili kufanikisha azma hiyo, ni wajibu wa Serikali kuimarisha nguvu ya uwezeshaji na uwekezaji katika kundi kubwa la wakulima wadogo waliopo vijijini.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages