Spika wa Bunge, Job Ndugai, amewasilisha bungeni takwimu za umri na kiwango cha elimu cha wabunge wote ambapo wenye Shahada za Uzamivu na Uzamili ni 161 kwa Bunge zima.
Ndugai alisema hayo jana, baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kutoa hoja ya kuahirisha Bunge, ambapo alisema katika takwimu hizo, Chama cha Wananchi (CUF) wanazo 14, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) 31 na Chama Cha Mapinduzi (CCM) 114.
Aidha, Spika Ndugai pamoja na mambo mengine, alisema hakuna Bunge limewahi kuwa na wasomi wengi kuzidi hili la 11 tangu nchi ipate uhuru mwaka 1961.
Katika takwimu zake hizo, amemtaja Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Bulembo (CCM), kuwa ndiye mbunge mwenye umri mdogo kuliko wote, akiwa na miaka 27, huku mbunge mwenye umri mkubwa kuliko wote akiwa na miaka 74, lakini hata hivyo, hakumtaja ila alisema; “ila leo hayupo.”
“Jana niliwaambia nitafanya zoezi kidogo la takwimu za wasomi ya kuona bunge letu likoje kiusomi, nimefanya ‘homework’ yangu, nitataja wachache, maana baadhi ya watu wanapenda kuliita bunge hili bunge la vijana, lakini baada ya takwimu hizi wabunge wenye umri wa miaka 40 kwenda mbele ni asilimia 80 ya wabunge wote.
“Kwa hiyo haya maneno ya kusema hili bunge la vijana siyo kweli, wakati mwingine ujana wakati mwingine ni ya ujumla sana, mtu anaweza akafikiri bado kumbe umri umeshaenda,” alisema Spika.
Alisema kwa upande wa kundi la Viti Maalumu, kwa kuanzia ameangalia takwimu za elimu ya sekondari kwenda mbele na kwamba elimu ya msingi ameiacha hadi siku nyingine.
“Elimu ya sekondari kwa Viti Maalumu wote ni 24, katika hao 24 CUF wako watano, Chadema watano, CCM 14, wenye cheti na stashahada CUF wanne, Chadema wanane na CCM 16,” alisema.
Spika Ndugai alisema wenye Shahada na kuendelea, Viti Maalumu CUF mmoja, Chadema 23, CCM 32, upande wa Shahada ya Uzamivu jumla 11, CCM 10 na mmoja Chadema, na kuongeza kuwa takwimu hizo zinasaidia wale wanaosema CCM haina wabunge wasomi, kwani bado CCM inatamba.
“Maprofesa tunao saba na wote saba ni wa CCM, PhD kwa wabunge wote humu ni 29, moja CUF, moja Chadema na 27 CCM, maana yake watu kwenye mitandao ooh CCM imejaza vihiyo mara eeh ehh, sasa takwimu hizo,” alisema Ndugai.
“Kwa ujumla wake wako baadhi wanasema Bunge hili ndiyo Bunge ambalo tangu historia halijawahi kutokea la namna hii kwa aina hii ya elimu niliyoieleza hili ni bunge la 11 tangu tupate uhuru, hakuna bunge limewahi kuwa na wasomi wengi kuzidi hili bunge la 11, huo ndio ukweli wenyewe na ndiyo hali halisi.
“Nilikuwa naangalia kule Buyungu kwa Mheshimiwa Chiza (Mbunge wa Buyungu, Christopher Chiza) wagombea wale wa CCM walikuwa kama 22, waligombea kwa CCM wote ni wahitimu wa vyuo vikuu, hiyo inakupa picha ya nchi sasa na inakoelekea, yaani kama Buyungu hali ni hiyo kwa vyovyote vile na kwingine nako kutakuwa kumechangamka,” alisema Spika Ndugai.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇