Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga (kulia) akimuonesha kitu Mwenyekiti wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali Waadiventista Wasabato (ATAPE), Bw. Fredy Manento, wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Uwekezaji la Chama hicho lililofanyika Mjini Bariadi Septemba 13, 2018.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga akifungua Kongamano la Uwekezaji la Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali Waadiventista Wasabato (ATAPE), kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka, lililofanyika Mjini Bariadi Septemba 13, 2018.
Mwenyekiti wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali Waadiventista Wasabato (ATAPE) Taifa, Bw. Fredy Manento, akitoa taarifa ya Chama hicho wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Uwekezaji la Chama hicho lililofanyika Mjini Bariadi Septemba 13, 2018.
Baadhi ya Wanachama wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali Waadiventista Wasabato (ATAPE), wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga (hayupo pichan) wakati akifungua Kongamano la Uwekezaji la Chama hicho lililofanyika Mjini Bariadi Septemba 13, 2018.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga (katikati) akiwasikiliza viongozi wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali Waadiventista Wasabato (ATAPE), mara baada ya kufungua Kongamano la Uwekezaji la Chama hicho kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka, lililofanyika Mjini Bariadi Septemba 13, 2018.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga (mwenye skafu) akiangalia bidhaa zinazotengenezwa na kuuzwa na Wanachama wa wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali Waadiventista Wasabato (ATAPE) kabla ya kufungua Kongamano la Uwekezaji la Chama hicho lililofanyika Mjini Bariadi Septemba 13, 2018.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga (mwenye skafu) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali Waadiventista Wasabato (ATAPE) na Wanakwaya ya Shamaliwa SDA Choir kutoka jijini Mwanza, baada ya kufungua Kongamano la Uwekezaji la Chama hicho lililofanyika Mjini Bariadi Septemba 13, 2018.
Na Stella Kalinga, Simiyu
Serikali mkoani Simiyu imesema imeandaa mazingira wezeshi kwa wawekezaji katika Fursa mbalimbali za uwekezaji ikiwemo viwanda, kilimo na teknolojia, ambapo imejipanga kutoa ardhi bure kwa wawekezaji walio tayari kuwekeza mkoani humo.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Wilaya ya Bariadi Mhe. Festo Kiswaga ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa huo , Mhe. Anthony Mtaka katika Ufunguzi wa Kongamano la Uwekezaji la Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali Waadiventista Wasabato (ATAPE), lililofanyika Mjini Bariadi Septemba 13, 2018.
Kiswaga amesema mkoa huo ni mkoa wenye ajenda ya maendeleo, hivyo umejipanga katika kuwawekea mazingira mazuri wawekezaji katika fursa mbalimbali za uwekezaji mkoani humo, ikiwa ni pamoja na sekta ya viwanda, kilimo, tekonolojia mbalimbali, uchimbaji wa visima na fursa nyingine, ili kufikia lengo la kuufanya mkoa huo kuwa katika nafasi nzuri kiuchumi.
“Mkoa wa Simiyu una fursa nyingi mkifika hapa chagueni tu sehemu mje kuwekeza, mtu atakayekuja kujenga kiwanda kikubwa, kizuri ardhi tutampa bure, sisi tutamuuliza tu kwamba tuandike jina gani kwenye hati na tutamkabidhi hati yake, kwa hiyo ATAPE pelekeni salamu kwa wawekezaji wenzenu kuwa ardhi ya uwekezeaji Simiyu ni bure, ninyi mtafute mtaji tu” alisema Kiswaga.
Ameongeza kuwa wawekezaji wote watakaowekeza mkoani Simiyu watapata soko la uhakika la bidhaa zao, huku akibainisha kuwa mkoa wa Simiyu na mikoa inayouzunguka ina wakazi wasiopungua milioni 10 ambao watakuwa wanunuzi wakubwa wa bidhaa zao watakazozalisha.
Aidha, Kiswaga ametoa wito kwa wawekezaji wote wakiwemo ambao ni wanachama wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali Waadiventista Wasabato (ATAPE), kuwekeza katika ujenzi wa hoteli na hosteli katika Eneo la Nyakabindi mahali ulipo Uwanja wa Nanenane Halmashauri ya Mji wa Bariadi ili kukabiliana na changamoto ya malazi.
Katika hatua nyingine Kiswaga ametoa wito kwa Taasisi za Madhehebu ya Dini kuiga mfano wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali Waadiventista Wasabato (ATAPE) katika kuwajenga waumini wao kiroho na kuwaimarisha kiuchumi, ili Taasisi kama hizo zitumike kama madaraja kuwavusha waumini wao kueleka katika Uchumi wa Kati.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali Waadiventista Wasabato (ATAPE), Bw. Fredy Manento amesema pamoja na kutoa huduma za kiroho ATAPE inatoa mafunzo ya ujasiriamali, imeweza kuwafikia zaidi ya wananchi 20,000 kupitia huduma za afya za bure na imewekeza zaidi ya shilingi milioni 639 katika miradi mbalimbali.
Makamu Mwenyekiti wa ATAPE Taifa (Upande wa Uwekezaji) Dkt. Dastan Kabiaro amesema katika uwekezaji huo ATAPE imeanza na kilimo ambapo imeshanunua jumla ya ekari 10,250 katika mikoa ya Tanga, Iringa, Pwani , Njombe na inatarajia kupata eneo jingine katika Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kilimo cha miwa ya sukari.
“ ATAPE imeanza kuwekeza katika kilimo,baadaye tutaenda kwenye maeneo mengine ambayo tumeshaanza kama maji, tutatoa visima \Tanzania nzima kwenye maeneo yote ambayo hayana maji; katika kilimo tumeanza kuchukua ardhi na kuiendeleza mpaka sasa tuna ekari 10,250, tumeendeleza ardhi hiyo kwa asilimia 10 na tunaendelea kuiendelea ardhi hiyo” alisema.
Mwenyekiti wa ATAPE Kanda ya Bariadi, Bi. Mariam Manyangu amesema mkoa wa Simiyu una wanachama takribani 80, ambao miongoni mwao ni watalaam katika fani mbalimbali pamoja na wafanyabiashara na wanaendelea kuhamasisha waumini wengi kujiunga na chama hicho, ili kujenga waumini imara kiuchumi watakaoweza kuendesha maisha yao na kuchangia kazi ya Mungu.
ATAPE ni kifupi cha Association Of Tanzania Adventist Proffessionals and Enterpreneurs -Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali Waadiventista Wasabato)-ambacho kilianzishwa mwaka 1999 kwa lengo kuwafanya Wanataaluma na Wajasiriamali watumie talanta zao kwa faida ya Jamii, Kanisa na kazi ya Mungu.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇