Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Singida Mhandisi Leonard Kapongo (kushoto), akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (kulia), wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa pamoja kilichopo wilayani Manyoni, mkoani Singida.
NA WUUM, SINGIDA
SERIKALI imesema imeshaanza kutoa misamaha ya kodi kwa mikataba ya ujenzi na matengenezo ya miradi ya maendeleo ikiwemo barabara, viwanja vya ndege na madaraja ambayo ilitakiwa kusamehewa kulipa kodi ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati akikagua hatua za ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa pamoja (One Stop Inspection Station), wilayani Manyoni mkoani Singida, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amesema kuwa mradi huo umechelewa kukamilika kutokana na mkandarasi kutopata msamaha wa kodi kama jinsi ilivyopangwa na hivyo kuathiri mtiririko wa fedha katika utekelezaji wa wake.
"Serikali imeanza kutekeleza misamaha ya kodi iliyokwama katika miradi inayoendelea na inayotarajiwa kuanza hapa nchini ikiwemo huu mradi na mingine mingi", amesema Waziri Mhandisi Kamwelwe.
Mhandisi Kamwelwe amemtaka mkandarasi wa Kampuni ya Impresa di Construction Ing E. Mantovani S. p. A con socio unico Via Belgio anayejenga kituo hicho kuhakikisha anakamilisha mradi huo ndani ya muda aliyoomba kuongezewa kwani hataongezewa muda mwingine.
"Nahitaji kituo hichi kikamilike ifikapo mwezi Februari mwakani, kwani haya ni maazimio ya pamoja ya nchi za wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kupunguza ucheleweshwaji wa usafirishaji wa mizigo kupitia barabara ya kati kuelekea nchi jirani", amesisitiza Mhandisi Kamwelwe.
Aidha, Waziri Kamwelwe ameeleza kuwa ukamilikaji wa vituo hivyo utapunguza muda na gharama za usafirishaji wa mizigo kupitia barabara ya Ukanda wa Kati (Central Corridor) kwani hadi sasa magari makubwa yanasimama vituo 31 kutokea Dar es Salaam hadi mipaka ya Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Awali akitoa taarifa ya mradi kwa Waziri huyo, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Singida Mhandisi Leonard Kapongo ameeleza kuwa maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho cha Manyoni umefikia asilimia 60 na ujenzi huo unaenda sambamba na ujenzi wa kituo kilichopo Nyakanazi mkoani Kagera.
Ameongeza kuwa ujenzi wa kituo hicho utahusisha uwekaji wa mizani ya mwendo, ofisi za Mamlaka ya Mapato (TRA), Polisi, Uhamiaji, kituo cha mapumziko na mafunzo kwa wasafirishaji, maegesho ya magari makubwa na nyumba za watumishi.
Mradi wa ujenzi wa vituo vikuu vya ukaguzi wa pamoja wa magari makubwa yanayoenda nje ya nchi unahusisha vituo vitatu ambavyo ni Vigwaza, Manyoni na Nyakanazi kwa umbali wa takribani kilomita 500 kutoka kituo kimoja hadi kingine ikiwa na lengo la kuondoa msongamano wa magari makubwa kwenye vituo vilivyopo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (wa pili kulia), akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Singida Mhandisi Leonard Kapongo (wa pili kushoto), wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa pamoja katika kijiji cha Muhalala, wilayani Manyoni, mkoani humo.(PICHA NA WUUM)
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇