LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Sep 25, 2018

SERIKALI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA WADAU KUBORESHA ELIMU NCHINI

Na Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.
Serikali imesema itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo nchini ili kuhakikisha kila mtoto wa kitanzania anapata elimu bora.

Hayo yameelezwa leo Jijini Dodoma na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wadau wa Elimu wa kujadili mafanikio na changamoto za elimu nchini.

“Mkutano huu ni muhimu sababu unapitia na kujadili mafanikio na changamoto katika sekta ya elimu na kutoa mapendekezo ya changamoto hizo ili kuboresha sekta hii,” amesema Prof. Ndalichako.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kutumia mapendekezo yanayotolewa na wadau wa maendeleo ya elimu nchini ili kuhakikisha hakuna mtoto wa Kitanzania anaachwa nyuma katika kupata elimu bora mijini na vijijini.

Amesema, Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa na mafanikio makubwa katika sekta ya elimu ambapo imefanikiwa kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari, mafunzo kwa mbalimbali kwa walimu, walimu wamepangiwa kazi kulingana na uhitaji pamoja na kuendelea kuwaajiri.

Vile vile Wadhibiti Ubora wa Elimu wamewezeshwa kwa kununuliwa magari na pikipiki ili kuzifikia shule kwa urahisi.

Prof. Ndalichako amewataka wadau hao kuutumia mkutano huo kujadili na kutoa mapendekezo ya namna ya kuimarisha ufundishaji wa masomo ya sayansi, kuunganisha elimu ya nadharia na vitendo, mafunzo ya walimu, elimu yenye usawa mijini na vijijini pamoja na mahudhurio shuleni.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo amesema mkutano huo umehusisha wadau mbalimbali wa elimu hapa nchini zikiwemo taasisi za utafiti, wadau wa maendeleo ya elimu, maafisa elimu pamoja na wanafunzi ambapo kwa pamoja watajadili mafanikio na changamoto katika sekta ya elimu na kutoa mapendekezo ya namna ya kukabiliana na changamoto hizo.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages