NA K-VIS BLOG/Khalfan Said
MKUU wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi amewataka Madaktari wanaopatiwa mafunzo ya jinsi ya kufanya tathmini kwa mfanyakazi aliyeumia au kuugua mahala pa kazi, kutenda kazi kwa weledi na kwa haraka ili kuharakisha utoaji wa fidia.
Mkuu wa Mkoa alitoa rai hiyo leo Septemba 24, 2018 wakati akifungua mafunzo ya siku tano kwa madakatari na watoa huduma za afya kutoka mikoa ya Singida, Dodoma, Kigoma na Tabora kwenye chuo cha Uhasibu Singida.
“Katika kutoa fidia kwa mfanyakazi aliyepata madhara mahala pa kazi hakuna njoo kesho….njoo kesho, bali ni kumhudumia Mfanyakazi huyo kwa haraka ili aweze kupata fidia yake kutokana na madhara aliyoyapata kwa wakati na ninyi madaktari ndio wenye jukumu kubwa la kuhakikisha mnafanya kazi kwa weledi na kwa haraka.” Alisema.
Dkt. Nchimbi alisema, katika suala la utoaji fidia, Madaktari ni sawa na mahakimu, na wanayo dhamana kubwa sana kwani mapendekezo yao ndiyo yatatoa muongozo kwa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, kuamua ni kiwango gani ambacho muathirika anapaswa kufidiwa au kutofidiwa kabisa.
“Kwa nafasi yenu Madaktari na kwa taaluma yenu mnafahamu sana namna ya kuwahudumia wahitaji wenu, lakini vile vile mnavyofanya katika tiba nyingine, huwezi kumtibu au kuwa na uhakika ni tiba ya namna gani mgonjwa anapaswa kupewa mpaka uwe na uelewa sahihi na ndio maana leo mko hapa ili muwe na uelewa sahihi, mtakapotoka hapa hatutarajii mseme sijui, sina uhakika, hayo siyo maneno ambayo tunataka yatoke kwenye vichwa vyenu baada ya mafunzo haya.
Alisema ni jambo zuri kwa madaktari wote baada ya kupatiwa mafunzo wawe na uelewa sahihi na wa namna moja, ili wote wakibadilishana uzoefu au taarifa, wakute kwamba wote wanapata huduma ambayo ina uelewa mmojana hayatakuwa maamuzi ya utashi binafsi wa daktari bali yawe maamuzi ya kitaalamu nay a haki.
Akizungumza wakati wa ukaribisho, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi WCF, Masha Mshomba alisema, mafunzo haya ya madaktari ni muendelezo wa mpango wa Mfuko kutoa mafunzo kwa wadau mbalimbali kuhusu shughuli za Mfuko na miongoni mwa wadau wakubwa wa Mfuko ni Madaktari.
“Jukumu kuu la Mfuko ni kupokea madai na kulipa mafao ya Fidia na hadi sasa tuna mwaka wa pili tukitekeleza jukumu hilo la msingi na nikuhakikishie kwamba tumekuwa tukilitekeleza na limeleta tofauti sana kati ya hali iliyokuwepo kabla ya kuanzishwa kwa Mfuko kwa maana ya malipo ya fidia yameongezeka sana na katika miaka miwili tu hii malipo ya fidia kwa wafanyakazi yamefikia shilingi Bilioni 4.5.” Alisema Bw. Mshomba.
Alisema, mafunzo haya yanalengo la kujenga uwezo kwa madaktari katika kufanya tathmini ya Mfanyakazi aliyeumia au kuugua mahala pa kazi ili hatimaye Mfanyakazi aweze kulipwa fidia stahiki.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Raskazi Muragila, alisema Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi una muda mfupi sana, umeanzishwa mwaka 2015 na utendaji rasmi umeanza mwaka 2016 kwa hivyo una miaka miwili tu hadi sasa, na ni wazi kwamba katika kipindi hiki kifupi, wafanyakazi wengi bado hawana uelewa kuhusu Mfuko huu, lakini pia wale wanaofanya tathmini (Madaktari) nao pia hawana uelewa wa kutosha kuhusu namna wanavyoweza kutimiza wajibu wao katika suala zima la ulipaji fidia.
“Naupongeza Mfuko kwa hatua iliyochukua ya kuendelea kutoa mafunzo kwa wadau mbalimbali na ningeuomba Mfuko uwatembelee pia wafanyakazi wenyewe na waajiri ili wote wawe na uelewa wa pamoja.” Alisema.
Mafunzo hayo yanaendeshwa na wataalamu kutoka Taasisi ya Tiba Moi na Mfuko wa Fidia kwa wafanyakazi, yatahusu Sheria ya Fidia kwa wafanyakazi na shughuli za Mfuko kwa ujumla, mchakato wa kupokea madai ya fidia, jinsi ya kufanya tathmini ya Mfanyakazi aliyeumia au kuugua kutokana na kazi..
|
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇