Serikali ya Tanzania imetoa agizo la kukamatwa na kufikishwa mahakamani, watoto wa mitaani, maarufu kama ombaomba, kwa kutumia sharia inayozuia utoro mashuleni.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Joseph Kakunda ambaye pamoja na kuashiria tatizo la ombaomba nchini humo, amewaagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri chini ya usimamizi wa wakuu wa mikoa kupitia kamati za ulinzi na usalama kuwakamata watoto wote ambao huzagaa mitaani wakiombaomba pamoja na wazazi wao na kisha kuwashtaki mahakamani chini ya sheria ya elimu ya mwaka 78 inayokataza utoro shuleni.
Kakunda ametoa agizo hilo mapema leo bungeni katika mkutano wa 12 alipokuwa akijibu swali la mbunge wa eneo la Kiembe Samaki Zanzibar, Ibrahim Raza na kuwataka wananchi kutumia fursa zilizowekwa na serikali kwa ajili ya kujikwamua na umaskini ikiwemo sera ya elimu bure. Awali mbunge Ibrahim Raza alikuwa ameiuliza swali serikali kwamba, ni lini itachukua hatua ya kuwaondoa watoto ombaomba jijini Dar es Salaa? Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Joseph Kakunda amesema kuwa, ombaomba wengi wanakwenda mji huo kutokana na kuwepo vivutio vingi vinavyowapa nafasi ya kupata fedha. Kwa mujibu wa Kakunda, serikali imebaini kwamba wapo watu wazima wanaowatumia watoto wadogo kuomba, na hivyo ametaka kutiwa mbaroni watoto wote ombaomba na kufikishwa mahakamani.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇