Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, raia wa kawaida nchini Yemen ndio wahanga wakuu wa mashambulio ya kijeshi ya Saudi Arabia na washirika wake.
Antonio Guterres amesema hayo alipokuwa akizungumzia matukio ya Yemen na kueleza kwamba, raia wa Yemen ndio walioathirika zaidi na vita dhidi ya nchi hiyo hususan mashambulio ya anga ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aidha amebainisha kwamba, Yemen inashuhudia maafa makubwa kabisa ya kibinadamu ulimwenguni.
Matamshi hayo yanatolewa katika hali ambayo, asasi mbalimbali za misaada ya kibinadamu zimekuwa zikitangaza kuwa, nchi ya Yemen inakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu kutokana na kukosekana huduma muhimu kama chakula na dawa.
Saudi Arabia ikisaidiwa na Marekani, utawala haramu wa Israel, Imarati na nchi nyingine kadhaa iliivamia kijeshi Yemen mwezi Machi mwaka 2015, na hadi sasa maelfu ya raia wasio na hatia wa nchi hiyo wameuawa na mamilioni ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.
Aidha mbali na mauaji, mzingiro mkubwa wa Saudi Arabia na waitifaki wake dhidi ya Yemen umeifanya nchi hiyo maskini ya Kiarabu ikabiliwe na hali mbaya ya uhaba mkubwa wa chakula, dawa na kukumbwa na milipuko ya magonjwa ya aina mbalimbali.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇