Ijumaa usiku jeshi la Marekani lilitangaza kwamba limeendesha maneva ya askari wa muungano wa kijeshi unaoongozwa na nchi hiyo huko Syria na ambao unadaiwa kuwa dhidi ya magaidi wa Daesh.
Jeshi la Marekani limetangaza kwamba maneva hiyo ya siku ya Ijumaa ilifanyika katika upana wa karibu kilometa 110 katika viunga vya kambi ya kijeshi ya al-Tanf nchini Syria. Baada ya Marekani kuunda muungano wa kimataifa unaodaiwa kuwa dhidi ya Daesh (ISIS) ililivamia eneo hilo na kuanzisha hapo kambi yake ya kijeshi. Pamela Spencer, mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa nchini Norway anasema: "Kambi ya kijeshi ya Marekani ya al-Tanf ni miongoni mwa kambi za kijeshi za nchi hiyo katika eneo la magharibi mwa Asia." Kuanzishwa kambi hiyo ya kijeshi kulitokana na matukio ya kusonga mbele jeshi la Syria katika nyuga mbalimbali dhidi ya magaidi, ambapo Marekani na kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi, iliunda kambi hiyo ili kuvuruga mafanikio ya kijeshi ya Syria dhidi ya magaidi. Suala hilo limekuwa likizingatiwa sana na wataalamu wa masuala ya kisiasa hususan katika siku za hivi karibuni. Ushindi wa jeshi la Syria katika uwanja wa vita, umeweka wazi hatima ya matukio ya nchi hiyo. Kwa maneno mengine ni kwamba, matukio mapya ya kijeshi nchini humo yameandaa mazingira bora kwa ajili ya kushindwa kikamilifu makundi ya kigaidi.
Serikali ya Damascus na washirika wake, ambao wanahusika katika matukio ya Syria, wanaendelea kubana nafasi ya maadui wa nchi hiyo. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana maadui wakaanzisha njama zenye lengo la kubadilisha hali ya mambo katika uwanja wa vita, ambapo makelele na propaganda za hivi sasa za Marekani kuilenga Syria, zinatekelezwa kwa lengo hilo. Kwa kushadidisha propaganda hizo dhidi ya Syria, serikali ya Marekani kwa mara nyingine inaandaa anga ya kutekeleza shambulizi la kijeshi dhidi ya nchi hiyo, kupitia uongo na hadaa kwamba jeshi la serikali ya Damascus limetumia silaha za kemikali dhidi ya raia. Harakati hizo za Marekani dhidi ya Syria zinatolewa katika hali ambayo, jeshi la nchi hiyo limepata ushindi mkubwa dhidi ya magaidi, kama ambavyo pia limeazimia kutekeleza operesheni kabambe dhidi ya magaidi katika mkoa wa Idlib ili kutoa pigo la kuangamiza na la mwisho dhidi ya magaidi hao. Eneo hilo ni lenye nafasi ya kistratijia na hivyo operesheni za jeshi la Syria katika maeneo hayo, ni utangulizi wa ukombozi kamili wa nchi hiyo kutokana na uwepo wa magaidi. Tunaweza kusema kuwa, kukamilishwa operesheni za jeshi la Syria dhidi ya magaidi, kumewatia wasi wasi mkubwa waungaji mkono wao hususan Marekani, kutokana na kushindwa kikamilifu vibaraka wao (magaidi) nchini humo.
Katika mazingira hayo, Marekani inatumia visingizio tofauti kwa ajili ya kufanya shambulizi jingine dhidi ya jeshi la Syria. Kwa mujibu wa gazeti la Raialyoum, serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani, inahisi kushindwa katika vita vyake nchini Syria, na ili kuendelea kuhalalisha uwepo wa askari wake katika ardhi ya nchi hiyo, Washington inataka kuingia katika vita vya muda mfupi na serikali ya Damascus, ili kwa njia hiyo iweze kudumisha kwa muda mrefu visingizio bandia vya mgogoro wa nchi hiyo ya Kiarabu. Hata hivyo matukio ya Syria yanaonyesha kwamba, nchi hiyo pamoja na washirika wake wanaounda mrengo wa muqawama katika eneo la Mashariki ya Kati, si tu kwamba hawatishiki na vitisho na njama za Marekani, bali wameazimia kuwatokomeza kikamilifu wanachama wa kigaidi nchini humo sambamba na kuhitimisha uingiliaji na uvamizi wa Washington ndani ya nchi hiyo. Aidha ushindi wa mrengo wa muqawama dhidi ya wavamizi katika vita vya Syria, unajiri huku baadhi ya madola ya Ulaya washirika wa Marekani yakikiri ukweli huo, kama ambavyo si mbali pia hata viongozi wa serikali ya Washington nao watalazimika kukiri ukweli huo. Ni wazi kuwa harakati za kijeshi za Marekani hazitokuwa na faida yoyote ghairi ya kushindwa kwingine kwa viongozi wa nchi hiyo ya kibeberu duniani.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇