Klabu ya soka ya Simba imemtangaza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa kuwa mgeni rasmi kwenye mchezo wa tamasha la 'Simba Day' dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana Agosti 8, 2018.
Akiongea na wanahabari Agosti 3, 2018, msemaji wa timu hiyo Haji Manara, amethibitisha kuwa tayari Waziri mkuu ameshakubali ombi lao na kuahidi atakuwepo uwanjani kuwaongoza mashabiki wa Simba katika tamasha lao lenye shughuli mbalimbali ikiwemo kutambulishwa kwa wachezaji wapya.
''Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekubali ombi letu, na ninaomba nitangaze rasmi kuwa yeye ndio atakuwa mgeni rasmi kwenye tamasha letu la 'Simba Day' akiongoza shughuli zote ambazo zitafanyika siku hiyo'', - amesema.
Mbali na kumtangaza mgeni rasmi, Manara amewataka mashabiki wa timu hiyo kutojihusisha na masuala ya kugushi tiketi kwani wao kama klabu wamejidhatiti kuhakikisha watu wa aina hiyo hawapati mwanya ndio maana suala la usimamizi wa tiketi uwanjani wamelikabidhi kwa Suma JKT.
Aidha Manara amesema kikosi cha Simba kitatua nchini Jumatatu ya Agosti 6 kikitokea Uturuki ambako kimeweka kambi ya maandalizi ya msimu wa 2018/19. Pia siku hiyo Simba watatambulisha jezi zao mpya za nyumbani na ugenini msimu huu.
|
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇