Wafuasi wasiopungua 28 wa mrengo wa upinzani nchini Zimbabwe wamepelekwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka ya kuzusha vurugu na machafuko baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi mkuu.
Washtakiwa hao ambao wote ni wafuasi wa chama cha upinzani cha MDC wanakabiliwa na mashtaka ya kuzusha vurugu na machafuko wakipinga matokeo ya uchaguzi.
Mawakili wa wafuasi wa mrengo huo wa upinzani wanasema kuwa, wateja wao ambao walitiwa mbaroni siku ya Jumamosi waandamwa wameshtakiwa katika fremu ya siasa za serikali za kuwatisha wapinzani.
Wapinzani hao wanapelekwa mahakamani katika hali ambayo, Rais Emmerson Mnangagwa ambaye ameshinda kiti cha Urais amewataka wananchi wa nchi hiyo kudumisha amani na usalama.
Nelson Chamisa Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe aliyegombea kwa tiketi ya chama cha MDC amesisitiza kuwa, katu hatayakubali matokeo ya uchaguzi wa rais akisema ni ya "uongo".
Uchaguzi wa kwanza wa rais baada ya miaka 37 ya utawala wa Robert Mugabe ulifanyika nchini Zimbabwe tarehe 30 Julai. Katika uchaguzi huo, Rais Emmerson Mnangagwa alishinda kwa asilimia 50.8 ya kura akifuatiwa na mgombea wa chama cha MDC Nelson Chamisa aliyepata asilimia 44.3 ya kura zote.
Kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa Rais nchini Zimbabwe kumefuatiwa na wimbi la machafuko na mapigano ambayo hadi sasa yamesha sababisha vifo vya watu sita.
Vyama vya upinzani nchini Zimbabwe vinaituhumu Tume ya Uchaguzi kwamba, ilikipendelea chama tawala cha ZANU-PF katika uchaguzi huo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇