LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Aug 28, 2018

UWANJA WA NDEGE WA DUBAI WASHAMBULIWA KWA KOMBORA LA ANSWARULLAH

Kikosi cha jeshi la anga kwa kushirikiana na Haraekati ya Wananchi ya Answarullah nchini Yemen, kimeshambulia uwanja wa ndege wa Dubai nchini Imarati kwa kutumia kombora aina ya Samad 3.
Naibu Msemaji wa Jeshi la Yemen, Aziz Rashid ameliambia Shirika la Habari la Sputnik kwamba, operesheni iliyofanywa jana jioni nchini Imarati, hususan kwa kuushambulia uwanja wa ndege wa Dubai, ina lengo la kutoa onyo jingine hasa baada ya kushambuliwa Shirika la Mafuta la Saudi Arabia Aramco. Itakumbukwa kuwa mwezi Juni mwaka huu jeshi la Yemen na kwa kutumia ndege isiyo na rubani ilishambulia kituo cha kusafishia mafuta cha Shirika la Mafuta la Aramco nchini Saudia, ambapo Riyadh ilikiri kuteketea kituo hicho. Katika indhari yake jioni ya jana, Aziz Rashid, Naibu Msemaji wa Jeshi la Yemen ameongeza kwamba, licha ya vita dhidi ya Yemen kuwa vya muda mrefu, jeshi la nchi hiyo limeweza kuwa na makombora ya balestiki na ndege zisizo na rubani na kwamba sasa maeneo ya kiuchumi na kijeshi ya adui yataanza kushambuliwa.
Msemaji wa Jeshi la Yemen Sharf Luqman
Wakati huo huo, Msemaji wa Jeshi la Yemen Sharf Luqman amezungumzia shambulio la jana dhidi ya uwanja wa ndege wa Dubai nchini Imarati na kuongeza kwamba, maeneo yote ya nchi hiyo yako katika shabaha ya jeshi na vikosi vya Yemen. Luqman amefafanua kuwa, makombora na ndege zisizo na rubani, zinaweza kushambulia maeneo muhimu ya Imarati, licha ya serikali ya nchi hiyo kuzidisha hatua za kiusalama. Itakumbukwa kuwa tarehe 26 Julai mwaka huu jeshi la Yemen na harakati ya Answarullah, lilishambulia pia kwa kombora aina ya Samad 3, uwanja wa ndege wa Abu Dhabi, nchini Imarati. Uwezo wa jeshi la Yemen na harakati ya wananchi, inazidi kuongezeka licha ya nchi hiyo kuzingirwa kila upande na Saudia, Imarati na waitifaki wao.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages