Emmerson Mnangagwa amechaguliwa kuwa rais wa Zimbabwe katika uchaguzi wa kwanza ambao haukumuhusisha rais wa kwanza wa nchi hiyo Robert Mugabe aliyetawala nchi hiyo kwa muda wa miaka 37. Baada ya kutangazwa matokeo rasmi ya uchaguzi huo wa Jumatatu nchi hiyo imetumbukia katika ghasia za kisiasa huku wapinzani wakidai kuwepo wizi wa kura.
Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Zimbabwe (ZEC), Mnangagwa wa chama cha ZANU-PF ameshinda kwa kupata asilimia 50.8 ya kura zote dhidi ya mpinzani wake Nelson Chamisa kutoka MDC aliyepata asilimia 44.3 ya kura zote. Chamisa alikuwa ametoa ahadi za kujenga upya miundo msingi ya kiuchumi ya nchi hiyo, kujenga reli ya kasi na kuhakikisha nchi hiyo inakuwa mwenyeji wa michezo ya olimpiki.
Chamisa ambaye pia alikuwa na uungaji mkono wa rais wa zamani wa nchi hiyo, Robert Mugabe, hakuweza kupata kura za kutosha kumuangusha Mnangagwa. Uchaguzi wa Julai 30 ulikuwa wa kwanza kufanyika nchini Zimbabwe bila Mugabe kuwa mgombea tokea nchi hiyo ijinyakulie uhuru mwaka 1980. Baada ya utawala wa miongoni karibu minne, Mugabe alilazimishwa na jeshi kuondoka madarakani mwezi Novemba mwaka jana.
Pamoja na kuwa uchaguzi huo ulikuwa na waangalizi wa kimataifa, baada ya matokeo kutangazwa wafuasi wa upinzani wamemiminika mitaani wakidai kuwa kumefanyika wizi wa kura.
Chamisa wa chama cha MDC pia naye amepinga matokeo ya uchaguzi na kuyataja kuwa bandia. Wanajeshi wa Zimbabwe wamezima ghasia hizo ambapo imearifiwa kuwa watu sita wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika kipindi cha siku chache zilizopita. Kuhusiana na hili Waziri wa Mambo ya Ndani wa Zimbabwe Obert Mpofu amesema: "Serikali haitastahamili maandamano. Wapinzani wanatujaribu lakini wanafanya kosa kubwa."
Sambamba na msimamo huo wa serikali, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetaka uchunguzi ufanyike kuhusu namna jeshi la Zimbabwe lilivyokandamiza maandamano ya wapinzani. Amnesty imesema kutumia jeshi kusimamia usalama baada ya uchaguzi Zimbabwe ni ukiukaji wa uhuru wa maoni.
Kufuatia ghasia hizo, Rais Mnangagwa wa Zimbabwe ametoa wito kwa wananchi kudumisha umoja kufuatia ghasia zilizoibuka baada ya tume ya uchaguzi kumtangaza mshindi katika uchaguzi uliofanyika wiki hii.
Katika ujumbe wake kupitia ukurasa wake wa Twitter, Mnangagwa amesema: "Huu ni mwanzi mpya na tunapaswa kuungana. Tumepata ushindi kwa uadilifu na uwazo na hakuna chochote cha kuficha."
Katika kampeni zake za uchaguzi Mnangagwa, ambaye alikuwa miongoni mwa washirika wakubwa wa Mugabe katika mapambana ya uhuru wa Zimbabwe, alisema atafanya mabadiliko makubwa akichaguliwa. Aidha aliahidi kubuni nafasi za ajira sambamba na marekebisho katika sekta ya uchumi wa nchi hiyo. Ahadi hizo na Mnangagwa zilitolewa katika hali ambayo nchi hiyo inakabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi, ukosefu wa ajira, umasikini na ufisadi wa kifedha. Kwa mujibu wa baadhi ya takwimu, karibu nusu ya Wazimbabwe hawana kazi na robo tatu ya watu wana pato la chini ya dola tano kwa siku. Katika kipindi ambacho Mnangagwa alikuwa rais wa muda baada ya Mugabe kutimuliwa, hakuweza kuboresha hali ya kiuchumi lakini sasa ameazimia kuimarisha uhusiano na nchi za kigeni na kuvutia wawekezaji sambamba na kuleta marekebisho ili kuboresha uchumi wa nchi hiyo.
Uhuru wa kisiasa ni kati ya matakwa ya wananchi wa Zimbabwe na Mnagagwa ameahidi kuheshimu takwa hilo la wananchi. Lakini wapinzani wanaamini kuwa Mnangagwa ataendeleza sera za chama tawala cha ZANU-PF na hivyo utawala wake hautatofutiana sana na ule wa Mugabe.
Kwa hivyo itabidi Mnangagwa aweze kuchukua hatua za kuwahakikishia Wazimbabwe kuwa ataleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi. Kwa sasa itabidi Wazimbabwe wasubiri na wampe muda rais wao mpya ili iweze kubainika iwapo atatekeleza ahadi zake au la.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇