LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 29, 2018

WAZIRI MKUU MAJALIWA AWAKOSHA WANANCHI WA MANISPAA YA KIGOMA-UJIJI; NI BAADA YA KUAGIZA WATAFITI WA ZAO LA CHIKICHI KUHAMIA MKOANI HUMO

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zito Kabwe katika mkutano wa hadhara aliouhutubia kwenye uwanja wa Kawawa katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, Julai 28, 2018
 NA K-VIS BLOG/Ofisi ya Waziri Mkuu

WANANCHI wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma-Ujiji, wamemkubali Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kufuatia uingiliaji kati kuhusu zao la Chikichi (Vigazi), ambalo hutoa mafula ya Mawese (Palm Oil).

Wananchi hao wamefurahishwa na uamuzi wa Waziri Mkuu wa kuitaka Wizara Kilimo na Mifugo, kuhakikisha watumishi wa kituo cha utafiti wa Michikichi cha Bagamoyo wanahamishiwa Mkoani Kigoma  ifikapo mwezi Agosti, 2018 isipokuwa wale wanaohusika na utafiti wa zao la minazi tu.

“Zao la Chikichi linalimwa Kigoma iweje utafiti ufanyiwe Bagamoyo, Waziri nakuagiza watumishi hao wanaohusika na masuala ya utafiti wa zao la Chikichi wahamie hapa Kigoma” Waziri Mkuu aliagiza katika kikao kazi alichofanya wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kufufua zao la Chikichi Mkoani Kigoma.

“Kwakweli ninayo furaha sana, tumelima ngazi (chikichi) kwa muda mrefu sana na kwa kutumia utaalamu wetu kidogo wa kuzaliwa, sasa uamuzi huu wa Waziri Mkuu wa kutuletea utalamu katika utafiti wa  zao hili ili liwe na manufaa zaidi ni mzuri” alisema Bwana Juma Dunia wa kijiji cha Mahembe.

Mwananchi mwingine Bw. Zigigwa Juma kutoka Kijiji cha Msimba yeye alibainisha hatua hii ya Serikali kuingilia kati kilio cha wana Kigoma kutaka itupie macho kwenye zao hili kuu la kiuchumi Mkoani kwetu kama ilivyo kwa mazao ya Kahawa, Chain a Pamba kwa mikoa mingine ni hatua ya kupongezwa.” Alisema.

Hata Mbunge wa Kigoma Mjini Mhe. Zitto Kabwe, naye kwa muda mrefu alikuwa anahamasisha wananchi kuhusu zao hilo la Chikichi kwenye eneo la bonde la Mto Mungonya, lakini pia kuitaka Serikali kuelekeza nguvu zake ili kuhakikisha Mkoa wa Kigoma unatoa kwa kiwango cha juu mafuta ya Mawese ambayo ndiyo hutumika kutengenezea mafuta ya kula kama vile Korie.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni ya kufufua zao la Michikichi (Vigazi), Julai 27, Mkoani Kigoma, Mhe. Kassim Majaliwa pia aliagiza kuanzishwa kwa kituo cha utafiti wa zao hilo katika chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Kihinga kilichoko Kata ya Mungonya Wilaya ya Kigoma Vijijini mkoani Kigoma kwa kuwa ndiko zao la Michikichi linalimwa kwa wingi.

Amesema Serikali imedhamiria kumaliza changamoto ya upatikanaji wa mafuta ya kula nchini kwa kuhamasisha kilimo cha zao la michikichiki kwa sababu kila mwaka Serikali hutumia zaidi ya sh. bilioni 600 kwa ajili ya kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.

 Waziri Mkuu ameyasema hayo leo  (Jumamosi, Julai 28, 2018) wakati akizungumza na viongozi wa mkoa wa Kigoma, wadau wa zao la michikichi na wabunge wa mkoa wa Kigoma baada ya kuwasili mkoani hapa kwa ziara ya kikazi ya siku nne inayolenga kuhamasisha maendeleo na kilimo cha zao la Michikichi.

 Amesema Serikali haiwezi ikaendelea kutumia fedha nyingi za kigeni kuagiza mafuta ya kula kutoka nje wakati uwezo wa kulima michikichi na kuzalisha mafuta ya mawese kwa wingi tunao, hivyo amewataka viongozi wa Serikali wabadilike na wawafuate wakulima kwenye maeneo ya vijijini na wakawasimamie na kuwashauri namna bora ya kulima zao hilo.

 Aidha, ameagiza Wizara ya Kilimo ianze taratibu za kisheria za kukihamisha chuo cha Kihinga kutoka Wizara ya Elimu Sayansi ya Teknolojia kwenda wizara ya Kilimo ili shughuli za tafiti za zao la michikichi lifanyike kwa ufanisi.

 Pia, ameiagiza Wizara ya Kilimo kuwahamishia mkoani Kigoma watumishi wa kituo cha utafiti wa michikichi cha Bagamoyo ifikapo mwezi Agosti, 2018 isipokuwa wale wanaohusika na utafiti wa zao la minazi tu.

 Kadhalika, amewataka viongozi  wa mikoa yote inayolima michikichi waanzishe mashamba ya michikichiki ili waoneshe mfano kwa wananchi. “Serikali inataka kuona mabadiliko kwenye zao hili. Sioni umuhimu wa Taifa kuendelea kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi wakati uwezo wa kuzalisha ndani upo,”.

 Amesema Serikali inataka kuona mabadiliko ya zao hilo, hivyo amewaagiza maafisa ugani katika maeneo yote wanayolima zao hilo wakafualitie maendeleo ya zao hilo kwa ukaribu zaidi. Zao hili litasimamiwa kuanzia hatua za uandalizi wa mashamba, upatikanaji wa pembejeo na utafutaji wa masoko.

 Waziri Mkuu amewataka wananchi wote wa mkoa wa Kigoma pamoja na mikoa mingine inayolima michikichi, wahakikishe wanapanda michikichi kwa wingi kuanzia kwenye makazi yao na kwenye mashamba yote wanayolima mazao mengine ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

“Serikali imefanya maamuzi ya kumaliza tatizo la mafuta ya kula nchini, kila mmoja lazima awajibike katika kuinua zao la michikichi ili tuweze kuzalisha mafuta ya kutosha,” amesema.

 Waziri Mkuu amesema Serikali itafuatilia kwa umakini kuhakikisha zao la michikichi linalimwa kwa wingi na kuleta tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla. “Tutumie zao hili kama fursa ya kujikwamua na umasikini pamoja na maliza changamoto ya upatikanaji wa mafuta nchini,”.

AwaliNaibu Waziri wa Kilimo, Bw. Omary Mgumba alisema zao la mchikichiki ni muhimu katika ukuzaji wa uchumi wa nchini, hivyo ufufuaji wa zao hilo ni kichocheo cha viwanda kwa kuwa kutakuwa na uhakika wa upatikanaji wa malighafi, hivyo kuvutia wawekezaji.

 Amesema kiasi kikubwa cha zao hilo hutumika katika kuzalisha mafuta ya kula, sabuni, hivyo ameshauri kiwepo chuo cha utafiti wa zao la michikichi mkoani Kigoma ili kurahisisha shughuli za uzalishaji. Mafuta yatokanayo na zao la michikichi yana mahitaji makubwa kwa kuwa bei yake ni nafuu jambo linalowezesha watu wengi wakiwemo wa hali ya chini kuyatumia.

Kwa upande,wake Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emanuel Maganga aliishukuru Serikali kwa uamuzi wake wa kufufua zao la michikichi kwa kuwa linalenga kuinua uchumi wa Taifa.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Mke wa Waziri Mkuu Mary Majaliwa, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhadisi Hamad Masauni, Naibu Waziri wa Ujenzi, uchukuzi na Miundombinu, Mhandisi Atashasta Nditie, Naiubu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, Naibu Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI, Jpsephat Kakunda, Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba.

 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanaja wa Kawawa katika Manispaa ya Kigoma Ujiji Julai 28, 2018.

 Sehemu ya umati wa watu wa Manispaa ya Kigoma Ujiji wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipohutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Kawawa Julai 28, 2018
 Wananchi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji wakimshangilia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipohutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Kawawa Julai 28, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary wakiwapungia wananchi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji wakati walipoingia kwenye uwanja wa Kawawa mjini Kigoma ambako Waziri Mkuu alihutubia mkutano wa hadhara Julai 28, 2018. (PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages