Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi (kulia) akitoa mada wakati wa kikao na wafanyakazi wa Taasisi hiyo pamoja na viongozi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kilichofanyika kivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo uliopo jijini Dar es salaam.
NA MWANDISHI MAALUM
WAFANYAKAZI wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kutobweteka kutokana na mafanikio mazuri ya kutoa huduma bora za matibabu ya moyo wanayoyapata bali waendelee kujitoa katika kuokoa maisha ya wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.
Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na Mkurugenzi wa Tiba kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Doroth Gwajima alipokuwa akizungumza na wafanyakazi katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo uliopo Jijini Dar es Salaam.
Dkt. Gwajima alisema hivi sasa Taasisi hiyo imekuwa tegemeo kubwa kwa wagonjwa wa moyo kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati hivyo basi ufanyaji kazi kwa ufanisi utasaidia wananchi wengi kuendelea kupata huduma za matibabu ya moyo hapa nchini.
“Jamii ya Tanzania inatambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa na JKCI, nawasihi wafanyakazi msikubali changamoto yoyote ile inayowakabili ikaitoa Taasisi hii katika mstari wa mafanikio mliyoyapata”.
“Mtambue kuwa Taasisi hii ni mkombozi wa wagonjwa wenye matatizo ya moyo ambao hivi sasa hawaendi tena kutibiwa nje ya nchi wanatibiwa hapa nchini matibabu ya kibingwa ya magonjwa ya moyo”, alisema Gwajima.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Prof. Mohamed Janabi alisema Taasisi hiyo itaendelea kutoa huduma bora zaidi, kupunguza wagonjwa wanaoenda nje ya nchi kutibiwa magonjwa ya moyo pamoja na kushirikiana na Serikali katika kutekeleza majukumu yao ya kazi za kila siku.
“Taasisi imefanikiwa kufanya kazi kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa nne usiku, kwa kufanya hivyo tumeweza kuona wagonjwa wote wanaofika kwa ajili ya kupata matibabu kwa wakati na kupunguza msongamano wa wagonjwa”, alisema Prof. Janabi.
Tangu kuanzishwa kwa Taasisi hiyo mwaka 2015 idadi ya wagonjwa wanaotibiwa imekuwa ikiongezeka kutoka elfu kumi na tano kwa mwaka 2015 hadi kufikia wagonjwa 64,093 kwa mwaka 2017.
Mkurugenzi wa Tiba kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Doroth Gwajima akimkabidhi tuzo ya utendaji kazi bora wa Idara ya Magonjwa ya Moyo ambayo ni moja ya Kurugenzi tano za Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Kaimu Mkurugenzi wa Idara hiyo ambaye pia ni daktari bingwa wa Magonjwa ya Moyo Peter Kisenge. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi.
Mkurugenzi wa Tiba kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto Dkt. Doroth Gwajima akimkabidhi Tuzo ya utendaji kazi bora wa Kitengo cha manunuzi David Kakoti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika hafla fupi ya kuzipongeza Idara na Vitengo vilivyofanya kazi vizuri kwa kipindi cha miezi mitatu. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akimpongeza Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu Ghati Chacha kwa ajili ya utendaji kazi mzuri wa Kurugenzi ya Utawala na Fedha walioufanya kwa kipindi cha miezi mitatu wakati wa hafla fupi ya kuwapongeza washindi iliyofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo. Kulia ni Mkurugenzi wa Tiba kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Doroth Gwajima.
Mkurugenzi wa Tiba Tanzania Dkt. Doroth Gwajima akimkabidhi Tuzo daktari bingwa wa upasuaji wa Moyo Dkt. Evarist Nyawawa kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kutokana utendaji kazi bora wa kitengo cha upasuaji wa Moyo wakati wa kikao na wafanyakazi wa Taasisi hiyo pamoja na wawakilishi kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto jana katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo jijini Dar es Salaam.
(PICHA NA BRIGHTON JAMES –JKCI)
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇