LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 2, 2018

RAIS DK. MAGUFULI AWAAPISHA LEO NA KUWAPA MAAGIZO MAZITO VIONGOZI ALIOWATEUA JANA

Rais Dk. John Magufuli skimuapisha Kange Ligola kuwa Waziri wa Mambo ys Ndani ya Nchi, Ikulu jijini Dar es Salaam, leo.

Ikulu, Dar es Salaam.
Rais Dk. John  Magufuli leo Julai 2, 2018 amewaapisha viongozi aliowateua jana na kuatoa maagizo mazito, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Viongozi hao walioapishwa ni Mawaziri watatu, Naibu Mawaziri wawili, Makatibu Wakuu watatu, Naibu Makatibu Wakuu watatu na viongozi wengine wa taasisi na idara za Serikali.

Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ,Mawaziri, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Wabunge, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa dini na viongozi wa vyama vya siasa.

Walioapishwa ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji  Prof. Makame Mnyaa Mbarawa, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano - Mhandisi Isack Aloyce Kamwelwe, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Kangi Alphaxard Lugola, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mussa Ramadhani Sima na Naibu Waziri wa Kilimo Omary Tebweta Mgumba.

Wengine ni Katibu Mkuu Ikulu Dk. Moses Mpogole Kusiluka, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Meja Jenerali Jacob Gideon Kingu, Katibu Mkuu Uvuvi  Dk. Rashid Adam Tamatamah, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi - Kailima Ramadhani Kombey, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi  Mathias Bazi Banduguru na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo  Prof. Siza Donald Tumbo.

Pia Rais Magufuli amewaapisha Jaji Mbarouk Salim Mbarouk kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Thomas Bashite Mihayo kuwa Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Balozi Mstaafu Omary Ramadhani Mapuri kuwa Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Wengine ni Athuman Juma Kihamia kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC na  Mohamed Ali Ahmed kuwa Naibu Msajili wa vyama vya siasa.

Akizungumza baada ya kuwaapisha viongozi hao na pia kula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Harold Nsekela, Rais Magufuli amewataka viongozi hao kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa huku wakizingatia kutekeleza Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCMya mwaka 2015 na kuhakikisha wanatimiza matarajio ya Watanzania katika taasisi wanazoziongoza.

Rais Magufuli amemtaka Waziri wa Maji na Umwagiliaji Prof. Mbarawa kushughulikia kikamilifu matatizo ya maji ambayo bado yanawakabili Watanzania licha ya Serikali kupeleka fedha nyingi katika wizara hiyo, kwa kuhakikisha miradi yote iliyokuwa inasuasua inaendelezwa kwa kasi zaidi ikiwemo kusimamia vizuri Sh. Trilioni 1.2 ambazo Serikali imekopa kutoka India kwa ajili ya miradi ya maji katika mikoa 17.

Kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Rais Magufuli ameelezea kutoridhishwa na utendaji kazi wa wizara hiyo na hivyo amemtaka  Lugola kushughulikia matatizo yaliyopo katika wizara hiyo.

Matatizo hayo ni pamoja maelekezo ya Kamati ya Bunge iliyotaka hatua zichukuliwe dhidi ya mkataba wa ufungaji vifaa katika vituo 108 vya Polisi uliogharimu Sh. Bilioni 37, uagizaji wa magari 777 ya polisi ambayo yamekwama bandarini na baadhi yake kuonekana yametumika.

 Kashfa ya ununuzi wa sare za Polisi, uhaba wa magari katika Jeshi la Zimamoto, kudhibiti mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOsambayo hayana maslahi kwa Taifa.

 Utoaji wa vibali vya kazi kwa wageni na ongezeko kubwa la ajali za barabarani, ambapo amemtaka kuwawajibisha mara moja Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya na Mkuu wa Usalama wa Barabarani wa Mkoa huo kufuatia ajali 3 zilizotokea mkoani humo na kusababisha watu 40 kupoteza maisha ndani ya wiki mbili.

Kwa Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, Rais Magufuli amemtaka Mhandisi Kamwelwe kuhakikisha miradi mikubwa ya ujenzi ikiwemo barabara, reli, viwanja vya ndege, utengenezaji wa meli, barabara za juu na njia za mabasi yaendayo haraka Jijini Dar es Salaam inatekelezwa kwa kasi zaidi pamoja na kusimamia vizuri Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) na maendeleo ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

“Serikali imenunua ndege 7, nataka ieleweke hizi ni ndege za Serikali sio za ATCL, lakini lengo letu ni kuiwezesha ATCL ilete watalii wengi ili tunufaike na utalii, asilimia 70 ya watalii husafiri kwa ndege, kwa hiyo kwa kukosa ndege tunapata Watalii Milioni 1 tu kwa mwaka, wakati nchi za wenzetu ambao hawana vivutio vingi kama sisi mfano Misri wanapata Watalii zaidi ya Milioni 10 kwa mwaka” amesema Rais Magufuli.

Mapema akitoa salamu zake Waziri Mkuu Kassim Majaliwa  amewataka viongozi walioteuliwa kuuanza mwaka mpya wa fedha wa Serikali kwa kuhakikisha wanashirikiana na viongozi wengine Serikalinikutekeleza maagizo yaliyotolewa na Wabunge wakati wa vikao vya Bunge vilivyomalizika wiki iliyopita.

Rais Dk. John Magufuli akizungumza  baada ya kuwaapisha viongozi hao na pia kula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Harold Nsekela. Kutoka kushoto ni Katibu Mkuu wa CCM Dk. Bashiru Ally, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi na Wazazi Mkuu Kassim Majaliwa.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages