Madaktari bingwa wa upasuaji wa watoto kutoka Chuo Kikuu cha Alexandria nchini Misri wakifanya upasuaji kwa mmoja wa watoto ambaye ana tatizo kwenye mfumo wa chakula (Gastroeso Phageal Reflux) disease) kwa kushirikiana na madaktari bingwa wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH). Kulia ni Prof. Saber Mohamed Waheeb kutoka Misri, Dkt. Mwajabu Rashid Mbaga wa Muhimbili na Dkt. Mohamed Abdelmalak kutoka Misri wakifanya upasuaji.
NA MNH
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) inaendelea kupata mafanikio makubwa kutokana na kuboresha huduma za upasuaji wa watoto, huku ndani ya siku mbili watoto 24 wakiwa wamefanyiwa upasuaji.
Wataalamu wa upasuaji wa watoto wa Muhimbili wamesema idadi ya watoto wanaofikishwa katika hospitali hiyo kutokana na matatizo mbalimbali, inaeendelea kuongezeka kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Watoto waliofanyiwa upasuaji ni wale wenye matatizo mbalimbali wakiwamo waliozaliwa bila kuwa na njia ya haja kubwa na wengine wenye matatizo kwenye mfumo wa chakula na hewa.
Upasuaji wa watoto hao 24 umefanywa na wataalamu wa upasuaji wa watoto wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kushirikiana na madaktari bingwa wa upasuaji wa watoto kutoka Chuo Kikuu cha Alexandria nchini Misri.
Akizungumza leo katika mkutano na waandishi wa habari, Daktari Bingwa wa Watoto katika hospitali hiyo, Dkt. Mwajabu Rashid Mbaga amesema wataalamu wa muhimbili na wa Chuo Kikuu cha Alexandria nchini Misri wameshirikiana kufanya upasuaji mgumu (difficult cases) kwa watoto hao.
Dkt. Mbaga amesema upasuaji huo umekuwa ukifanywa mara kwa mara na wataalamu wa Muhimbili kwa muda mrefu na kwamba katika siku mbili wamekuwa na wataalamu wa Chuo Kikuu cha Alexandria kwa ajili ya kubadilisha uzoefu.
“Kuanzia Alhamisi hadi Ijumaa wiki hii tumekuwa na jopo la watalaamu wenzetu 10 wa upasuaji kutoka Chuo Kikuu cha Alexandra kilichopo Misri wakiongozwa na Prof. Saber Mohamed Waheeb mshauri mwelekezi katika upasuaji wa watoto na Dkt. Mohamed Abdelmalak Morsi bingwa wa upasuaji wa watoto,” amesema Dkt. Mbaga.
Kufanyika kwa upasuaji huo kumetokana na juhudi za uongozi wa Muhimbili kuimarisha miundombinu ya vyumba maalumu(exclusive operating theaters) vya upasuaji wa watoto.
Wakati huo huo, hospitali hiyo ilipokea watoto pacha walioungana ambao walizaliwa Julai 12, 2018 kwa njia ya kawaida wakati mama akiwa njiani kuelekea hospitalini huko Vigwaza Mkoani Pwani.
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto wa Muhimbili, Dkt. Petronilla Joseph Ngiloi amesema pacha hao wameungana sehemu ya tumbo na sehemu ya ndani na kwamba wanachangia INI tu huku viungo vingine kila mmoja akijitegemea.
“Watoto hawa walizaliwa na kilo mbili, lakini sasa wamefikisha kilo 4 na gramu 640. Tunategemea kuwafanyia upasuaji wa kuwatenganisha katika kipindi cha miezi mitatu hadi minne ijayo kuanzia sasa. Tumejiridhisha kwamba tutaweza kuwatenganisha sisi wenyewe hapahapa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili,” amesema Dkt. Ngiloi.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Muhimbili, Dkt. Julieth Magandi alishukuru jopo la wataalamu kutoka Misri kwa kushirikiana na wataalam wa hospitali hiyo kwa kuwa wamebadilishana uzoefu.
Madaktari na wataalamu wengine wakiendelea na upasuaji kwa mtoto mwenye tatizo kwenye mfumo wa chakula (Gastroeso Phageal Reflux disease).
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Mwajabu Rashid Mbaga (kushoto), Prof. Saber Mohamed Waheeb kutoka Misri (kushoto), Dkt. Mohamed Abdelmalak kutoka Misri (kulia) na Muuguzi msaidizi, Agness Charles wa Muhimbili (kulia) wakiendelea na upasuaji
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Mwajabu Rashid Mbaga (kushoto), Daktari Bingwa wa Nusu Kaputi, Dkt. Kareman Ibrahim kutoka Chuo Kikuu cha Alexandria nchini Misri na Muuguzi msaidizi, Agness Charles wa Muhimbili (kulia) wakiendelea na upasuaji katika hospitali
Dkt. Julieth Magandi wa Muhimbili akipokea zawadi kutoka kwa Prof. Saber Mohamed Waheeb wakati wa mkutano wa wataalamu hao na waandishi wa habari
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Mwajabu Rashid Mbaga akizungumza na waandishi wa habari leo baada ya wataalamu wa upasuaji wa watoto wa Muhimbili na wale wa Chuo Kikuu cha Alexandria nchini Misri kufanya upasuaji kwa watoto 24 wenye matatizo mbalimbali. Watoto hao wanaendelea vizuri baada ya kupatiwa huduma hiyo. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa MNH, Dkt. Julieth Magandi, Dkt. Petronilla Joseph Ngiloi wa MNH, Prof. Saber Mohamed Waheeb kutoka Misri, Dkt. Mohamed Abdelmalak kutoka Misri na Dkt. Ibrahimu Mkoma wa MNH.(PICHA NA JOHN STEPHENE WA MNH)
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇