Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imesema wavuvi wasiopungua 12 raia wa nchi hiyo wameuawa katika mapigano makali yanaoendelea kushuhudiwa kwa siku kadhaa sasa kati ya vikosi vya majini vya nchi hiyo na Uganda, katika maji ya Ziwa Edward.
Muhindo Kyakwa, afisa mwandamizi wa DRC katika eneo la Kivu Kaskazini ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, "Miili ya raia wetu 12 ingali inaolea katika maji ya Ziwa Edward, baada ya makabiliano makali baina ya askari wa majini wa Uganda na Kongo DR. Tumeshindwa kuziopoa maiti hizo kwa kuwa wanajeshi wa Uganda wanamfyatulia risasi mtu yeyote anayekaribia eneo hilo."
Awali serikali ya Kinshasa ilikuwa imedai kuwa, wavuvi 16 raia wa Kongo wametoweka katika maji ya Ziwa Edward.
Alkhamisi iliyopita, askari wanne na raia watatu wa Uganda waliripotiwa kuuawa katika mapigano hayo baina ya vikosi vya majini vya Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika maji ya Ziwa Edward.
Hujuma hiyo ilifanyika chini ya masaa 48 baada ya kikosi cha majini cha Uganda kuwatia mbaroni wavuvi 18 raia wa Kongo kikidai kuwa walikuwa wameingia katika maji ya nchi hiyo ndani ya Ziwa Edward.
Watu wasiopungua 30 aghalabu yao wakiwa wavuvi wanahofiwa kupoteza maisha katika makabiliano hayo baina ya wanajeshi wa majini wa Uganda wa DRC katika maji ya Ziwa Edward lililoko katika mpaka wa nchi mbili hizo jirani.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇