*Ataka apewe majina ya watakaokiuka agizo hilo
*Akataza magari ya Serikali kulala nyumbani kwa mtu
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Bahi mkoani Dodoma wanaoishi nje ya eneo lao la kazi wawe wamehamia ifikapo Julai 30, mwaka huu.
“Tunataka watumishi wa umma wawajibike na waishi katika vituo vyao vya kazi. Nawataka watumishi wote wa wilaya hii wanaoishi Dodoma wawe wamehamia hapa ifikapo Julai 30 mwaka huu na wasiohamia nipewe majina yao,” amesisitiza.
Pia ameagiza magari yote ya Serikali baada ya kuisha muda ya kazi yawe yameegeshwa kwenye ofisi za halmashauri na ni marufuku kwa magari hayo kulala nyumbani kwa mtu.
Ametoa maagizo hayo leo (Jumatano, Juni 27, 2018) wakati akizinduavituo 51 vya kufuatilia taarifa za hali ya hewa, vituo 15 vya haidrolojia, kanzidata ya taarifa za hali ya hewa na kituo cha operesheni na mawasiliano ya dharura wilayani Bahi, Dodoma.
Waziri Mkuu amesema Serikali inataka watumishi wote wa umma nchini waishi kwenye vituo vyao vya kazi ili waweze kuwahudumia wananchi kwa ukaribu katika maeneo husika.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bahi, Bibi. Rachel Chuwa aanzishe mradi wa upimaji wa viwanja na viuzwe kwa watumishi na wananchi kwa gharama nafuu.
Waziri Mkuu amesema ni vema wilaya hiyo ikachangamkia fursa ya Serikali kuhamia Dodoma kwa kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo nyumba za kuishi, hoteli na sehemu za burudani ili watumishi waliohamia Dodoma wapate sehemu za kujipumzisha pindi wamalizapo majukumu yao.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇