Ramadhani Maneno akiomba kura kabla ya uchaguzi mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Mkoani Pwani ambapo alishinda kuwa mwenyekiti Mpya Mkoani hapo.
Wajumbe wa mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Mkoani Pwani,wakifuatilia uchaguzi mkuu wa CCM Mkoani hapo uliofanyika kwenye ukumbi wa Filbert Bayi Kibaha.(picha na Mwamvua Mwinyi)
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
RAMADHANI Maneno amechaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa mkoa wa Pwani na kumdondosha mwenyekiti aliyekuwa akitetea kiti chake Mwinshehe Mlao ambae aliongoza nafasi hiyo kwa miaka kumi na Tano .
Aidha Hajji Jumaa ,amechaguliwa kuwa mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM Taifa ,kupitia mkoa wa Pwani.
Akisoma matokeo kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM mkoani hapo,msimamizi wa uchaguzi huo ,Frenk Haule ambae pia ni katibu uchumi na fedha Taifa na (MNEC),alimtangaza Maneno, ameshinda kwa kupata kura 402 dhidi ya Mlao aliejinyakulia kura 344 na Rehema Suleimani 19.
Alieleza idadi ya wapiga kura 768 ,zilizopigwa 768 kura zilizoharibika ni 3 kura halali 765 .
Kwa mamlaka aliyopewa pia ,Haule alimtangaza Hajji kuwa mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM Taifa kupitia Pwani kwa kupata kura 381 ,dhidi ya Rugemalila Rutatina aliyepata kura 246.
Wengine waliogombea nafasi nafasi hiyo walikuwa Robert Bundala Katuba aliyepigiwa kura 28, Zainab Gama 49 na Abdulkarim Shaha kura 56 .
Haule alisema katika nafasi ya wajumbe wa halmashauri kuu mkoa ambao walitakiwa wawili kila wilaya kwa wilaya ya Rufiji amechaguliwa Yusuph Mbonde na Hawa Mtopa.
Wilaya ya Mafia alichaguliwa Saidi Abeid na Fakhi Ally ,wilaya ya Kibaha Vijijini ameshinda Mwajuma Denge na Kulwa Abdallah.
Msimamizi huyo alisema wilaya ya Kibaha Mjini amechaguliwa Alice Kaijage na Catherine Katele.
Bagamoyo waligombea wanane ,walioshinda ni pamoja na Mwanaharusi Jaruf na Imam Madega na Kisarawe wagombea walikuwa sita walioshinda ni Tatu Kano na Pingu Betera.
Haule alielezea katika wilaya ya Kibiti amechaguliwa Mariam Mohammed na Amina Mapande na Mkuranga ni Hassan Dunda na Rehema Mazoea ambapo wamekuwa wajumbe wawili kuwakilisha halmashauri kuu Mkoa kutoka kwenye wilaya hizo.
Akishukuru wajumbe Maneno aliwahakikishia kusimamia utekelezaji wa ilani ya CCM ,na kuinua uchumi na maendeleo ya Mkoa.
Mbali ya hilo aliahidi kushirikiana na wadau kujenga ukumbi wa CCM mkoa ndani ya uongozi wake,ambao utakaosaidia kuondokana na kufanya mikutano mikubwa kwenye kumbi za kukodi .
Maneno hakusita kuomba ushirikiano kwa wanachama na viongozi wengine kuanzia ngazi ya chini ili kuimarisha chama .
Mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM Taifa -Pwani ,Hajji aliwashukuru wajumbe wote kwa umoja wao na kuahidi kusimamia maendeleo ya mkoa kwa kwenda kusikiliza kero kwa wananchi .
Alisema ni wakati wa viongozi wa chama kutoka maofisini na kuwafuata wananchi na wanachama ili kujua changamoto zao.
Hajji aliwataka wanaCCM mkoani hapo kuwa wamoja ,kushikamana kwa lengo la kukiletea ushindi chama hicho kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu 2020.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇