DODOMA, TANZANIA
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameitaka Benki
Kuu ya Tanzania (BOT) kudhibiti
matumizi ya fedha za kigeni katika biashara na huduma hapa nchini ili kulinda nguvu
ya fedha ya Tanzania na kukabiliana na uhalifu wa kifedha.
Mhe.
Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 13 Desemba, 2017 wakati akifungua tawi la
benki ya CRDB-LAPF Dodoma na kubainisha kuwa hatua hiyo itasaidia kuimarisha
uchumi wa nchi.
Aidha,
Mhe. Rais Magufuli ameitaka BOT kuongeza usimamizi wa benki zinazoendesha
shughuli zake hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha zinajiunga na mfumo wa
ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki na kufuatilia kwa ukaribu utendaji
wake wa kila siku ili ziwe na manufaa kwa nchi.
“Hivi
sasa kuna benki 58 hapa Tanzania, BOT ni lazima mzifuatilie kwa ukaribu benki
hizi, na zile zisizofanya vizuri chukueni hatua mara moja, ni bora tubakiwe na
benki chache kuliko kuwa na benki nyingi zinazofanya vibaya,
Pia
nataka mdhibiti matumizi ya Dola, hivi navyozungumza kuna Dola Milioni 1 zimekamatwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dar es
Salaam, hakuna maelezo yoyote juu ya kuingia fedha hizo, ni lazima tuwe makini”
amesisitiza
Mhe. Rais Magufuli.
Mhe.
Rais Magufuli ameipongeza benki ya CRDB kwa kuendeshwa kwa ufanisi tangu
ilipobinafsishwa kutoka Serikalini ambapo katika kipindi cha miaka 10 imelipa
kodi serikalini kiasi cha Shilingi Bilioni 800, imetoa ajira kwa Watanzania
3,200,imetoa gawio Serikalini la Shilingi Bilioni 19.5 mwaka huuna imetoa
mikopo yenye thamani ya Shilingi Trilioni 3.5 ambapo Shilingi Trilioni 1 kati
yake zimeelekezwa katika sekta ya viwanda na kilimo.
Kuhusu
kupungua kwa kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi Mhe. Rais Magufuli
amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali zitakazoongeza kasi hiyo zikiwemo
kupunguza kiwango cha kisheria cha sehemu ya amana za benki za biashara
kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu kutoka asilimi 10 hadi 8, kushusha riba ya
Benki Kuumara mbili kutoka asilimia 16 hadi 9, kutoa mikopo maalum kwa benki za
biashara, pamoja na Benki Kuu kununua fedha za kigeni kwenye soko la jumla la
benki ili kuongeza ukwasi wa shilingi kwenye uchumi.
“Kutokana
na hatua hizi nimeambiwa kuwa hali ya ukwasi imeanza kuimarika na kusaidia
kupunguza riba katika soko la fedha baina ya benki (IBCM rate) kutoka asilimia
13.69 Desemba 2016 hadi kufikia asilimia 3.29 Novemba 2017, pia riba katika
soko la dhamana za Serikali zimepungua kutoka wastani wa asilimia 15.12 hadi
8.76 katika kipindi hicho” amebainisha Mhe.
Rais Magufuli.
Mhe.
Rais Magufuli ametoa wito kwa benki zote nchini kuanzisha matawi ya benki
vijijini na kuwakopesha wajasiriamali ili waweze kuongeza uzalishaji hasa
kilimo na viwanda, na pia ametaka wananchi wanaopata mikopo wazingatie
kurejesha.
Mapema
katika maelezo yake Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Dkt. Charles Kimei amempongeza
Mhe. Raia Magufuli kwa juhudi kubwa za kuimarisha uchumi zikiwemo ujenzi wa
viwanda, ununuzi wa ndege, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ujenzi wa barabara za juu (Flyover) na ameahidi kuwa CRDB yenye matawi 469 na wateja 3,500,000
ikiwa ndio benki inayoongoza kwa mtandao mkubwa nchini, itaendelea kushirikiana
na Serikali katika kuwawezesha wajasiriamali na uwekezaji katika viwanda na
kilimo.
Dkt.
Charles Kimei na Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB Bw. Ally Laay wamekabidhi hundi ya
Shilingi Milioni 100 kwa Mhe. Rais Magufuli kwa ajili ya kuchangia huduma za
kijamii, na Mhe. Rais Magufuli amekabidhi hundi hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma
Dkt. Binilith Satano Mahenge kwa ajili ya ujenzi wa wodi katika hospitali ya
Mkoa Dodoma.
Ufunguzi
wa tawi la CRDB LAPF Dodoma umehudhuriwa na Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth
Magufuli, Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai, Naibu Spika Dkt. Tulia
Ackson, Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. John Samwel Malecela na Waziri wa Fedha na
Mipango Mhe. Philip Isdor Mpango.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇