LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Nov 9, 2017

RIDHIWANI AKERWA KUSUASUA KWA MIRADI YA MAENDELEO CHALINZE

Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze
MBUNGE wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete, amekerwa kwa kusuasua kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Chalinze mkoa wa Pwani, licha ya kuwa ya tatu nchini kwa ukusanyaji mzuri wa mapato ya ndani.

Kutokana na hilo amewataka wataalamu na watendaji wa halmashauri ya Chalinze kuacha visababu vinavyokwamisha kumaliza viporo vya miradi ya maendeleo vilivyopo tangu mwaka wa fedha 2016/2017.

Aidha ameeleza, halmashauri hiyo inakusanya zaidi ya milioni 300 kwa mwezi ambapo kwa miezi mitatu inafikia milioni 900 hadi bilioni moja lakini utekelezaji wa miradi umekua haukidhi mahitaji.

Pamoja na hilo, Ridhiwani ameitaka wakala wa barabara Vijijini na Mjini (TARURA) kuhakikisha wanashirikiana na madiwani wa kata ili waweze kupewa vipaombele vya mahitaji halisi ya barabara zinazohitajika kwasasa.

Akitoa rai hiyo ,wakati wa baraza la madiwani la kawaida la halmashauri hiyo,alieleza hiyo ni halmashauri moja wapo kati ya zinazofanya vizuri kimkoa na kitaifa lakini haifikii malengo yanayotakiwa.

Ridhiwani alisema atakuwa mkali kwa hilo na hatosita kulikemea hadi hapo halmashauri itakaposimama kushirikiana na matakwa ya madiwani kwa maslahi ya wananchi.

Alielezea hofu yake ikifikia 2020 watashindwa kuisemea ilani kwa kudorora kwa miradi kutokana na kupelekwa fedha chache kwenye miradi hiyo wakati fedha zipo.

Ridhiwani alisema kila eneo la mradi kwenye kabrasha limewekwa deshi ama bado ,na kudai kwa mwendo huo ni kuididimiza halmashauri.

Alieleza ifikie wakati wa kusimamia mapato ya ndani na miradi ya mendeleo kwa maslahi mapana ya wananchi na sio vinginevyo .

"Ikifikia hatua ya kuanza kusigana kutokana na matumizi ya fedha humu ndani kutakuwa hakukaliki ,ni wakati wa kufanya yale yenye tija kwa watanzania tuache mchezo kwenye fedha hizi"

"Kama fedha inapangwa kwenda kutekelezwa miradi kwanini isifanye kazi husika ,kwanini kila mradi haujamalizwa " haya masuala tuayaache haiwezekani kwenye kabrasha kila sehemu ya mradi ni deshi ,deshi jamani hatutafika kwa dizaini hii "alisema Ridhiwani.

Akizungumzia suala la TARURA alisema,ni changamoto kwani wamekuwa wakienda kujenga barabara kwenye kata mbalimbali bila kuwashirikisha madiwani wala wananchi.

Ridhiwani alisema zipo barabara zenye mahitaji makubwa kwa sasa zinazotakiwa kuboreshwa na kujengwa ili kuondoa kero kwa wananchi .

Alieleza ni lazima TARURA wafuate mahitaji na vipaombele vinavyotakiwa kuliko kujiamulia vipaombele vyao visivyokidhi malengo.

"Tofauti na ambavyo tulitegemea  tunashauri ikiwezekana tukutane na huyu mtendaji mkuu wa TARURA  Mkoa wa Pwani kama Taifa tuzungumze nae kuhusu barabara zetu za Chalinze na tujadiliane nini kifanyike" alisema Ridhiwani.


Alisema wamekua wakipanga miradi ya barabara ambayo inahitaji kutekelezwa lakini utekelezaji wake umekua ukisuasua changamoto ikiwa ni ushirikishwaji mdogo kati ya  ya TARURA, Halmashauri na baraza la madiwani.

Nae diwani wa kata ya Kibindu ,Suleimani Mkufya alisema katika kata yake barabara yenye urefu wa kilomita 12 TARURA wamejenga kilomita tano .

Walipohojiwa walidai kuwa fedha waliyopewa ni ya kilometa tatu na kilomita mbili wameongeza wenyewe.

Kauli hiyo ilizua utata kwa madiwani kwani wanashindwa kuelewa kwanini barabara hazikamiliki kwa wakati na pia utaratibu wa TARURA kuongeza kilometa zake fedha hizo wanazitoa kwenye mfuko upi.

Diwani wa kata ya Miono Juma Mpwimbwi alisema kilio chake kipo katika fedha za makusanyo ambapo zinapangiwa matumizi ambayo hayatekelezwi kwa wakati.

Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri hiyo Said  Zikatimu alisema kiasi cha sh.milioni 225 zilitengwa kwa ajili ya miradi ya barabara kwa mwaka wa fedha 2016/2017 na tayari baadhi ya miradi inaendelea kutekelezwa.

Kuhusu kusuasua kwa miradi alisema watahakikisha wanasimamia fedha zinazotengwa kwenda kwa wananchi zinaleta matokeo chanya.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages