Waziri Ummy Mwalimu |
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa pongezi za dhati kwa watoto wote waliopata ufaulu wa juu na kushika nafasi 10 bora kitaifa katika matokeo ya mtihani wa Darasa la Saba kwa mwaka 2017.
Aidha, kwa namna ya pekee Wizara inawapongeza wanafunzi 4 wa kike waliopata ufaulu wa juu na kuingia kwenye ushindani wa nafasi kumi bora kwa mwaka huu wa 2017, ukilinganisha na mwanafunzi 1 tu wa kike aliyeng’ara katika nafasi hizo kwa mwaka 2016.
Taarifa iliyotolewa na Wizara hiyo imesema wizara imetambua juhudi binafsi zilizofanywa na mwanafunzi wa kike Hadija A. Ally kutoka Shule ya Msingi Sir John ya jijini Tanga, ambaye ameshika nafasi ya kwanza kati ya wanafunzi 10 hodari kitaifa na pia Wizara inampongeza mwanafunzi aliyeshika nafasi ya pili, Naseem K. Said (Sir John, Tanga), nafasi ya sita ikishikiliwa na Insiya Kalimuddin (Sir John Tanga), na nafasi ya saba ikishikilikiwa na Colletha Masungwa wa St. Achileus, ya mkoani Kagera.
Kadhalika, Wizara imewapongeza wanafunzi wa kike na wakiume ambao wameonesha jitihada katika kutekeleza wajibu wao masomoni ikisema, hii inaonesha dhahiri walikuwa wasikivu kwa walimu wao, wazazi na walezi wao hivyo kuweza kupata matokeo mazuri.
Taarifa ya TECTA inaonesha kuwa ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 70.3 ya mwaka 2016 hadi asilimia 72.76 kwa mwaka 2017, sawa na ongezeko la asilimia 2.4; huu ni ushuhuda thabiti kuwa wadau wa watoto wameshirikiana na Serikali katika kuimarisha na kuboresha mazingira ya watoto kupata haki ya kuendelezwa na kumwezesha Mtoto wa kike na wa kiume kutimiza ndoto zake.
Juhudi zilizooneshwa na watoto hawa wa kike ni ishara ya matokeo mazuri ya utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kutoa fursa sawa kwa watoto wa kike na wa kiume katika kupata haki ya elimu. Wakati tukiendelea na utekelezaji wa kampeni ya “Mimi Msichana, Najitambua; Elimu ndio Mpango Mzima”, Wizara inatoa rai kwa watoto wote wa kike kutafakari matokeo ya mwaka ya huu ili kuwa chachu ya kujitambua na kukataa mimba za utotoni. Kama wanafunzi wa kike watajitambua na kujilinda, wataweza kusoma kwa ari kubwa kwa manufaa yao na kutumikia Taifa kwa uzalendo wa dhati.
Wizara inawataka watoto wote wa kike na wa kiume waelewe kuwa wamehitimu daraja moja, na bado wanalojukumu la kujiendeleza zaidi katika masomo ya sekondari na kwa wale ambao hawakupata ufaulu unaotosheleza wanayo nafasi ya kujiendeleza kupitia taaluma mbalimbali na stadi za maisha ili kupata maarifa yatakayowawezesha kutoa mchango katika juhudi za kufikia uchumi wa kati na wa viwanda.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇