Moja ya mali za Majembe Auction Mart Ltd |
Mali za kampuni maarufu ya udalali iliyowahi kutikisa nchi kutokana na kutokuwa na msalie mtume inapopewa tenda ya kukamata na kuuza mali za wadaiwa Majembe Auction Mart Ltd, ‘Vijana wa Kazi’ zinatarajiwa kupigwa mnada kufidia deni.
Habari zimeeleza kuwa, hatua hiyo imekuja baada ya mfanyabiashara maarufu nchini Frank Marealle kushinda kesi namba tisa ya mwaka 2014 ya ardhi, katika Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi Kanda ya Tanga dhidi ya Majembe Auction Mart Ltd.
Inaelezwa kuwa Marealle aliiburuza mahakamani Kampuni ya Majembe Auction Mart, baada ya kushinda dau katika mnada wa hadhara uliofanywa na kampuni hiyo mwaka 2012, wilayani Korogwe mkoani Tanga uliohusu eneo lenye ukubwa wa ekari 3000.
Chanzo cha habari hiyo kinasema Marealle baada ya kushinda dau hilo aliilipa Majembe Auction Mart kiasi cha zaidi ya sh. milioni 745 (sh. 745,054,487.83) kwa kufuata taratibu za mnada lakini kwa mujibu wa habari hizo Majembe, ambayo ilifanya kazi hiyo kwa udalali baada ya Mahakama kutoa amri eneo liuzwe haikuwasilisha fedha katika mamlaka husika.
Kufuatia hali hiyo, ikaonekana Marialle hakupewa haki zake kama mnunuzi halali wa eneo hilo, hivyo akalazimika kufungua kesi dhidi ya Majembe katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kitengo cha ardhi mwaka 2014.
Hatimaye Marealle alishinda kesi ambapo Oktoba 9 mwaka 2014 mahakama hiyo, ilitoa oda kwa dalali wa mahakama Chodry Kahema kuiruhusu kampuni ya udalali ya Lonzadu ya Moshi, kuuza mali za Majembe ili kurejesha fedha.
Oda hiyo ya mahakama pia iliitaka kampuni ya Majembe kuwasilisha hati yenye orodha ya mali zisizohamishika na kutokuthubutu kuuza, kuhamisha umiliki au kubadili umiliki wa mali hizo kwa aina yoyote.
Dalali Mussa Kahena amethibisha kampuni yake kupewa kazi ya kukamata mali za Majembe akisema keshokutwa Oktoba 6 mwaka huu atawasilisha ombi katika Mahakama Kuu ya Ardhi ya Tanzania Kanda ya Tanga kuomba mali za Majembe kuuzwa.
“Tutaomba kibari cha kuuza kwa sababu muda wa kuzikamata mali zake umepita na ameshindwa kulipa deni. Kinachofuata ni kuiomba mahakama ituruhusu sasa kupiga mnada wa hadhara,”alisema.
Alisema tayari kampuni ya udalali ya Lonzandu inashikilia nyumba mbili za kifahari za Majembe, moja iliyopo eneo la Mikocheni na nyingine ni nyumba namba nne iliyopo Mbezi Beach mtaa wa Seaview Drive.
“Tunataraji mnada kufanyika Oktoba 14 mwaka huu ili tuweze kukusanya fedha anayodaiwa.Tulimpa notisi ya siku 14 kwa mujibu wa sheria lakini Majembe ameshindwa kutii,”alisema Kahema.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇